Nuru FM

Mufindi yafungua fursa za uwekezaji, biashara, ajira

13 October 2026, 09:09

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dkt. Linda Salekwa akizungumzia kuhusu maonesho ya Mufindi Investment Forum and Expo 2026. Picha na Fredrick Siwale

Maonesho hayo yanaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuijenga Tanzania yenye uchumi imara na shindani, maendeleo jumuishi, ustawi wa wananchi na fursa zaidi za kiuchumi.

Na Fredrick Siwale

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, amewaalika wawekezaji, wafanyabiashara, wadau wa maendeleo na wananchi kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Mufindi kushiriki Maonesho ya Mufindi Investment Forum and Expo 2026, yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 16 hadi 20, 2026, katika viwanja vya Shule ya Msingi Wambi.

Akizungumza leo, ofisini kwake, Dkt. Salekwa amesema maonesho hayo yanalenga kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo Mufindi, kuwaunganisha wawekezaji na wadau wa biashara, pamoja na kutoa elimu itakayowawezesha washiriki kutambua na kutumia fursa katika sekta za viwanda, utalii, kilimo na biashara.

Kwa mtazamo huo, Mufindi Investment Forum and Expo ni fursa ya kugeuza rasilimali na uwezo wa wilaya katika kilimo, viwanda na utalii kuwa uwekezaji wenye tija, ajira na maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi.

Dkt. Salekwa ameeleza kuwa maonesho hayo yatazinduliwa Oktoba 16 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo, huku siku ya kilele na kufungwa kwa maonesho hayo, Oktoba 20, kukitarajiwa kufanywa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Kheri James.

Sauti ya DC Linda

Katika ratiba ya siku tano, kutakuwa na mijadala ya siku mbili itakayowakutanisha wadau kutoka sekta za biashara, uwekezaji, kilimo na utalii kujadili fursa zilizopo, changamoto na mikakati ya kukuza biashara. Mijadala hiyo itaambatana na elimu kuhusu uwekezaji na namna ya kutumia fursa zilizopo Mufindi kuchochea ukuaji wa uchumi.

Sauti ya DC Linda

Maonesho hayo yameandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi kwa kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) na wadau wengine. Dkt. Salekwa amesisitiza umuhimu wa wananchi na wadau kujitokeza kwa wingi, akieleza kuwa ushiriki wao utasaidia kuifanya Mufindi kuwa kitovu cha fursa, ubunifu, biashara na uwekezaji wenye manufaa kwa jamii na uchumi wa wilaya kwa ujumla.