Wachimbaji wafungiwa shughuli zao.
9 August 2021, 3:19 am
Na Mrisho Sadick:
Wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Kanegere namba mbili Wilayani Mbongwe Mkoani Geita ,wameiomba serikali kupitia Wizara ya Madini kuwasaidia kutatua changamoto ambayo inawakabili ya kufungiwa shughuli zao na ofisi ya madini mbogwe kwa muda wa zaidi ya siku sita sasa.
Wakizungumza na Storm FM Kijijini humo baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamelalamikia vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na Ofisi ya madini mkoa wa kimadini wa mbogwe kwa kuwafungia shughuli zao za uchimbaji pamoja na uchenjuaji wa madini ya dhahabu.
Mmiliki wa leseni katika eneo hilo Bw Katemi Walwa amesema Afisa madini amekuwa akiwatisha kuwafungulia kesi ya uhujumu uchumi pindi wanapodai haki zao nakwamba tangu waanze shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu hawajawahi kuacha kulipa mapato serikalini.
Afisa Madini wa Mkoa wa Kimadini Kahama ambae anakaimu na Mkoa mpya wa Kimadini wa Mbongwe ,Mhandisi Joseph Kumburu amekanusha madai ya kufunga shughuli za uchimbaji na uchenjuaji kuendelea ambapo amesema kumekuwepo na utoroshaji wa mifuko wa mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu, ndio sababu ya kuweka uthibiti wa kuwabana baadhi ya wachimbaji ambao wanakwepa kulipa kodi.