Askari magereza alalamikiwa kuharibu mali za ndani Geita
9 December 2024, 3:54 pm
Licha ya kampeni ya kimataifa ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, bado vitendo vya ukatili vimeendelea kujitokeza katika Jamii ambavyo vinasababisha athari mbalimbali kwenye Jamii.
Na: Evance Mlyakado – Geita
Mwanaume mmoja ambaye ni Askari wa Jeshi la magereza mkoani Geita amelalamikiwa kufanya uharibifu ndani ya nyumba ya Mariamu Williamu kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na ugomvi wa kifamilia.
Akizungumza na storm Fm Bi. Mariam Williamu ambaye ni mkazi wa mtaa wa Nyerere road amesema kuwa mwanaume huyo aliyefahamika kwa jina la Godfrey Michael ambaye ni Askari wa Jeshi la magereza hapa mkoani Geita anadaiwa kufanya uharibifu ndani ya nyumba hiyo usiku wa kuamkia leo Disemba 09, 2024.
Godfrey Komba ambaye ni baba mwenye nyumba amesema kuwa mpangaji wake anayemtambua ni Mariam Wiliamu na kwamba sio msumbufu huku akisema kuwa ugomvi wa wanafamilia hao hapo awali uliamuliwa na Afisa mtendaji wa mtaa huo kwa Godfrey Michael kuamuliwa kuondoka katika familia hiyo.
Kwa upande wake Methew Charles Nkwabi ambaye ni balozi wa shina namba 3 amesema kesi mbalimbali za familia hiyo zimekuwa zikimfikia huku Kamanda wa polisi jamii kata ya Kalangalala Patrick Paulo akibainisha kuwa kitendo kilichofanywa na Askari huyo ni kinyume na maadili ya kazi na kueleza taratibu zilizochukuliwa.
Baada ya taarifa kufikishwa katika uongozi wa Jeshi la Magereza hapa mkoani Geita, Maafisa kadhaa wa Jeshi hilo walifika katika familia hiyo wakiwa wameambatana na mtuhumiwa mwenyewe ili kujionea uharibifu wote ndani ya chumba hicho uliofanywa na Askari huyo kisha kumchukua Mariamu, Afande Godfrey ambaye ndiye mlalamikiwa na baadhi ya viongozi na mmiliki wa nyumba hiyo ili kwenda kuzungumzia suala hilo kwa viongozi wa juu kwani mwanamke huyo alidai fidia ya mali iliyoharibiwa.