Rashi eneo la Mabunduki yanufaisha kijiji cha Nyakagwe
2 September 2024, 1:31 pm
Geita ni mkoa ulioko kaskazini-magharibi mwa Tanzania ambao ni maarufu kwa uchimbaji wa madini ya dhahabu ambapo vijana wengi wamejiajiri hasa kupitia uchimbaji mdogo wa madini ili kuendesha maisha yao.
Na: Ester Mabula – Geita
Kijiji cha Nyakagwe kilichopo kata ya Butobela halmashauri ya wilaya ya Geita mkoani Geita kimenufaika na uwepo wa eneo dogo la uchimbaji madini ya dhahabu lijulikanao kwa jina la Mabunduki ambalo liligunduliwa na kuanza kazi Agosti 22, 2024.
Akizungumza na Storm FM Septemba 01, 2024 mwenyekiti wa kijiji cha Nyakagwe Daudi Lumala ameeleza juu ya gawio walilopata kuwa ni zaidi ya shilingi milioni 60 ambazo zimeelekezwa katika miradi ya maendeleo ya kijiji ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Katika hatua nyingine ametoa rai kwa wamiliki wa maeneo ya uchimbaji kuendelea kutoa gawio kwa kijiji ili kuweza kufanikisha maendeleo kama mwongozo wa sheria ya madini unavyoelekeza.
Ngusa Silvester ni Meneja wa eneo hilo ameeleza namna eneo hilo lilivyopatikana na kuanza kufanyiwa kazi sambamba na kutaja mikakati iliyopo ya kuliendeleza zaidi.
Baadhi ya wachimbaji akiwemo msimamizi wa eneo hilo wameeleza namna wanavonufaika na uwepo wa eneo hilo pamoja na kutoa ushauri kwa idara ya madini juu ya namna ya kuwasaidia kurahisisha shughuli hizo za uchimbaji