GGML yafadhili mafunzo kukabiliana na majanga ya moto
12 August 2024, 4:42 pm
Jumla ya watumishi 78 kutoka halmashauri ya mji wa Geita wamepewa mafunzo ya namna ya kukabiliana na majanga ya moto.
Na: Ester Mabula – Geita
Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya GGML iliyopo mkoani Geita, kwa kushirikiana na Jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Geita imetoa mafunzo kwa watendaji wa halmashauri ya mji wa Geita juu ya kukabiliana na majanga ya moto.
Akitoa mafunzo hayo leo Agosti 12, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya mji wa Geita, Kaimu kamanda wa Jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Geita mrakibu msaidizi wa Jeshi la zimamoto na uokoaji Edward Lukuba ameipongeza GGML kwa kuendelea kuiishi dhana yao ya usalama na kueleza kuwa wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha Jamii kuzingatia usalama huku akisisitiza kuwa jukumu la kujikinga na majanga ya moto ni la kila mmoja kwenye jamii.
Katika hatua nyingine Afisa Lukuba ametaja matukio ya moto ambayo yanaongoza kuripotiwa katika mkoa wa Geita.
Awali GGML ilitoa mafunzo kwa wanafunzi ambapo jumla ya wanafunzi waliopata elimu shule za sekondari ni 15,091 na walimu 2 kwa halmashauri ya mji na wilaya ya Geita, kama anavyobainisha kaimu afisa elimu sekondari Linda Marandu.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wenzake Valeria Lukoba ametoa shukrani kwa GGML na Jeshi la zimamoto na uokoaji kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia katika kazi zao za kila siku
Mafunzo yaliyotolewa ni sehemu ya mipango ya GGML katika kuchangia maendeleo ya jamii ambapo wamekuwa wakishirikiana na taasisi nyingine za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuhakikisha kuwa jamii inakuwa salama na yenye ustawi.