Dkt Biteko awaonya walioficha watoto wasiende shule
9 June 2024, 1:55 pm
Kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi zaidi ya 440 ambao wameshindwa kuripoti shule katika wilaya ya Bukombe serikali imeanza kutumia nguvu kuwatafuta popote walipo nakuwapeleka shule.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Doto Biteko ametoa maagizo ya watoto wote waliyofichwa wasiende shule kuhakikisha wanapelekwa haraka kwakuwa serikali imetumia fedha nyingi kuwekeza kwenye elimu kwa ajili yao.
Akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Jimbo lake la Bukombe katika Kata ya Bugelenga wilayani Bukombe Mkoani Geita jana Juni 07,2024 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Doto Biteko amesema hakuna sababu ya watoto wanaotakiwa kwenda shule kufichwa majumbani.
Awali mkuu wa wilaya ya Bukombe Paskasi Muragili amesema kuna idadi kubwa ya wanafunzi ambao wamefichwa wasiende shule nakwamba wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu walikuwa ni 7,532 na walioripoti hadi mwezi wa kwanza walikuwa ni 6,854 na ambao hawakuripoti hadi mwezi wa tatu walikuwa ni 678 na baada ya msako mkali wamefanikiwa kuwapata 229 bado 449 ambao hawajulikani walipo na msako unaendele.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt Festo Dugange akiwa kwenye mkutano huo amesema serikali imewekeza kwenye elimu fedha nyingi wilayani humo kwa kutoa zaidi ya Bilioni 9 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita wamesema msingi wa maendeleo ni mshikano nakwamba watumishi wote wa umma wapo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na si vinginevyo.