UWT Ludete yawapa tabasamu wanafunzi walioripoti bila sare
3 February 2024, 7:23 pm
Jamii yashauriwa kuendelea kuwasaidia wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira magumu ili waweze kutimiza ndoto zao.
Na Mrisho Sadick:
Wananchi kwa kushirikiana na Jumuiya ya umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kata ya Ludete wilayani Geita wamejitokeza kuwasaidia wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira magumu ikiwemo wale walioshindwa kumudu gharama za kununua sare za shule.
Wakizugumzia hatua ya kuwasaidia wanafunzi hao kupata sare za shule na taulo za kike Mwenyekiti wa UWT Kata ya LudeteĀ Frola Lubango na baadhi ya wananchi waliounga mkono jitihada hizo wamesema wanafunzi wengi wa vijijini wanakabiliwa na Changamoto rukuki na wasipo saidiwa huenda wakafifisha ndoto zao huku katibu wa umoja huo Renata Nestori akisema watoto wa kike ndio wanakabiliwa na changamoto nyingi zaidi.
Kwa upande wake Rahma Emmanuel Mkazi wa Kata ya Ludete aliyeambatana na UWT katika maadhimisho hayo ya miaka 47 ya CCM ameahidi kuwanunulia wanafunzi sare za shule na Baiskeli moja kwa mwanafunzi anaetembea umbali mrefu kwenda shule ya sekondari Mlando.
Madiwani wa viti maalumu Kutoka katika Kata hiyo Maimuna Mingisi na Antonia Lubadila wakiwa kwenye zoezi hilo wamempongeza Mwenyekiti wa UWT kwa uthubutu huo nakusema kuwa wanaadhimisha Miaka 47 ya kuzaliwa CCM kwa kusaidia wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira magumu huku wakimpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu.