Walimu wanyang’anywa madawati, wakaa chini Geita
25 January 2024, 5:52 pm
Kitendo cha walimu kunyang’anywa madawati waliyokuwa wakiyatumia kwenye ofisi yao kimezua mjadala.
Na Mrisho Shabani – Geita
Chama cha walimu Tanzania (CWT) wilayani Geita kimelaani kitendo cha serikali ya kijiji cha Nyansalala Kata ya Bukondo wilayani Geita cha kuwanyang’anya walimu madawati waliyokuwa wakiyatumia hali ambayo imewalazimu walimu hao kufanya shughuli zao wakiwa wamekaa chini.
Wakizungumzia changamoto hiyo baadhi ya walimu wa shule hiyo wamesema afisa Mtendaji wa kijiji hicho akiwa na wajumbe wa serikali ya kijiji na kamati ya shule walifika shuleni hapo nakuwataka walimu hao kupisha kwenye madawati kwa madai kuwa yanatakiwa kutumiwa na wanafunzi na si walimu.
Hata hivyo baada ya kumtafuta afisa mtendaji huyo amesema hilo ni agizo la halmashauri ya kijiji baada ya mwalimu mkuu wa shule hiyo kushindwa kutengeneza viti na meza kwa ajili ya walimu licha ya kuahidi kufikia januari 25 atakuwa amekamilisha kazi hiyo.
Kufuatia madai hayo Mwenyekiti wa chama cha Walimu Wilaya ya Geita Samwel Joseph amekemea vikali kitendo hicho huku akiziomba mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria.