Anusurika kichapo baada ya kukutwa na nguo aliyoiba
30 July 2024, 6:31 pm
Licha ya Jeshi la polisi kuendelea kuzuia matukio ya kujichukulia sheria mkononi kwa kujeruhi watuhumiwa, bado wananchi wameendelea kujichukulia sheria mkononi.
Na: Amon Mwakalobo – Geita
Mwanaume mmoja mkazi wa Bomani, mtaa wa Katoma halmashauri ya mji wa Geita anayejulikana kwa jina moja la Mafanikio amenusurika kichapo kutoka kwa watu wenye hasira kali siku ya Ijumaa Julai 26, 2024 majira ya saa mbili usiku baada ya kukamatwa mtaa wa Msalala road maeneo ya Msufini na mwanaume aliyejitambulisha kwa jina la Jacob Felix akimtuhumu kumuibia nguo zake.
Akizungumza na Storm FM Jacob amesema ameibiwa mara mbili nyumbani kwake hasa suruali zake na masufuria ya mkewe ambapo moja ya suruali yake ndo ambayo amemkamamta nayo akiwa amevaa.
Kwa upande wake Bw. Mafanikio anayetuhumiwa ameeleza kuwa nguo hizo alinunua huku akikana kuhusika na wizi huo
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo ambao ndio waliomuokoa Mafanikio kutoka kwenye kichapo cha wananchi wametetea na kusema wanamfahamu na hana tabia za udokozi isipokuwa inawezekana aliuziwa na watu walioiba
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Msalala road ambako ndiko tukio hilo limetokea Sostenes Kalist amewataka wananchi kuacha mara moja tabia ya kununua vitu mikononi kwa watu na endapo wakikamatwa navyo wao ndio watahesabika kuwa ni wezi na kuchukuliwa hatua.