Watoto 2,578 Wapatiwa Chanjo Mkoani Geita
11 May 2021, 6:01 pm
Na Mrisho Sadick:
Watoto 2578 waliochini ya umri wa miaka mitano wamepatiwa chanjo katika mkoa wa Geita kwenye wiki ya Maadhimisho ya chanjo ya Umoja wa Mataifa(UN) idadi ambayo ni mkubwa ukilinganisha na lengo la serikali ya mkoa huo ya kutoa chanjo kwa watoto 1266.
Maadhimisho ya wiki ya chanjo hufanyika kuanzia April 24 hadi 30 ya kila mwaka ambapo wizara ya Afya Maendeleo ya jamii Jinsia,Wazee na watoto hutoa huduma ya chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano ili kuwakinga magonjwa mbalimbali hasa katika kipindi cha ukuaji wao.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Mratibu wa Chanjo mkoa wa Geita Bi Wille Luhangija amesema zoezi hilo liliendeshwa kwa watoto ambao walikuwa hawajapata chanjo zikiwemo za surua,polio,kupooza na pepopunda.
Luhangija,alisema chanjo imekuwa ikileta mafanikio makubwa ambapo kwa kipindi kirefu tatizo la watoto kupooza limepungua kwa kiasi kikubwa.
Aidha,akitolea mfano katika mkoa wa Geita,Mratibu wa chanjo Wille Luhangija alisema, ni zaidi ya miaka kumi mkoa huo haujawahi kupokea kesi ya motto aliyepooza,hivyo akaitaka jamii kuzingatia kuwapatia chanjo watoto ili kuwajengea kinga ya mwili itayokabiliana na magonjwa yanayoweza kuwaathiri katika kipindi cha makuzi yao.
Alisema,chanjo kwa watoto hazina madhara isipokuwa humsaidia mtoto kuwa na Afya bora na kuisaidia sarikali na jamii kuepukana na matumizi ya gharama kubwa kushughulikia afya katika makuzi yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mhandisi Robert Gabriel amesema serikali ya mkoa itahakikisha inazingatia maelekezo ya serikali ya kutoa chanjo kwa watoto sababa na kuboresha huduma za Afya kwa wananchi.
Alisema mkakati wa serikali ni kuhakikisha kila kijiji,mtaa unakuwa na zahanati na kata inakuwa na kituo cha Afya lengo la serikali ni kuwasogezea huduma wananchi hasa akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.