DC Geita akemea migogoro ya wakulima na wafugaji
22 June 2024, 3:33 pm
Migogoro ya wakulima na wafugaji hutajwa kuwa chanzo cha kurudisha nyuma maendeleo katika jamii za wafugaji na wakulima, jambo ambalo viongozi hukemea vikali.
Na: Kale Chongela – Geita
Wakazi wa mtaa wa Mpomvu kata ya Mtakuja mjini Geita wameiomba serikali ya wilaya ya Geita kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji kufuatia kuwepo kwa hali ya baadhi ya wakulima kupigwa na wafugaji.
Wameeleza hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Juni 21, 2024 mbele ya mkuu wa wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba ambapo baadhi ya wakulima wameeleza kuwa pamekuwepo na changamoto ya baadhi yao kupigwa na wafugaji hasa wanapo wabaini kuwa wamelisha mifugo kwenye mashamba yao.
Mkurugenzi wa halmashauri ya mji Geita Bw. Yefred Myenzi ametumia fursa hiyo kuwataka wafugaji kuzigatia kanuni bora za ufugaji ili kuondoa changamoto hizo.
Mkuu wa wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba amemuugiza afisa mifugo kufika katika eneo hilo na kutatua mgogoro huo kabla haujaleta madhara makubwa kati ya wakulima na wafugaji.