Wawili wafariki dunia baada ya kufukiwa na udongo Magenge
7 June 2024, 11:54 am
Uchimbaji mdogo wa madini kwenye maeneo yasiyo rasmi katika baadhi ya maeneo mkoani Geita bado ni kitendawili ambacho kinapelekea changamoto ikiwemo wachimbaji kupoteza maisha kutokana na ubovu wa miundombinu.
Na: Edga Rwendru – Geita
Watu wawili wamepoteza maisha baada ya kufukiwa na udongo wakati wakiendelea na shughuli za uchimbaji wa madini katika machimbo yasiyo rasmi eneo la Magenge wilayani na mkoani Geita.
Tukio hilo limetokea Juni 04, 2024 majira ya asubuhi. Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Afisa zimamoto na uokoaji mkoa wa Geita Wambura Fide amesema tukio la watu hao kufukiwa na udongo limetokea katika eneo lililokatazwa kuendesha shughuli za uchimbaji kutokana na eneo hilo kutokuwa na usalama.
Mwenyekiti wa kijiji Mathias Deo na diwani wa kata hiyo Edward Misungwi wameeleza kuwa wamiliki wa leseni za uchimbaji wa madini wanatakiwa kubainisha maeneo ya kufanyia kazi kwani uongozi ulikuwa hauna taarifa kuwa eneo hilo limekatazwa na haukuwa na taarifa kama eneo hilo kuna mmiliki mwenye leseni ya utafiti.
Kwa upande wake Abdul Joseph Stanslausi ambaye ni Mmiliki wa leseni hiyo amesema kabla ya kutokea kwa ajali hiyo alikuwa ametoa taarifa kwa viongozi husika.