Maonesho ya biashara, viwanda na kilimo kuanza mwezi Mei Geita
11 April 2024, 5:49 pm
Katika kukuza fursa za kibiashara , kilimo na viwanda Mkoa wa Geita huandaa kila mwaka maonesho yanayogusa sekta hizo ili wahusika waweze kuyatumia kujijenga zaidi.
Na Mrisho Sadick – Geita
Zaidi ya wajasiriamali 200 na makampuni makubwa kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajia kushiriki katika maonesho ya tano ya Biashara , viwanda na Kilimo Mkoani Geita.
Akizungumza na waandishi wa Habari Mratibu wa maonesho hayo Raphael Siyantemi amesema maonesho yanatarajia kuanza mei 22 hadi juni 2 mwaka huu katika viwanja vya maonesho vya EPZ Bombambili mjini Geita.
Meneja wa Shirika la viwanda vidogo SIDO Mkoa wa Geita Nina Nchimbi amesema maonesho hayo yamekuwa na mafanikio makubwa kwa wajasiriamali huku akiwataka wawekezaji kuchangamkia fursa hiyo kwakuwa Mkoa wa Geita una fursa nyingi za kiuchumi katika sekta za Uchimbaji wa Madini, Kilimo , Uvuvi na Ufugaji.
Mwenyekiti wa Chemba ya wafanyabiashara Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amesema miongoni mwa washiriki wa maonesho hayo ni wajasiriamali Kutoka visiwani Zanzibar nakwamba kutakuwa na fursa mbalimbali zitakazo wawezesha wajasiriamali kujiinua kiuchumi.