Tukuze Utalii wa ndani sisi wenyewe
15 April 2021, 6:23 pm
Na Mrisho Sadick:
Katika kukuza utalii wa ndani baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari Mkoani Geita wameungana kwa pamoja kuchangia ziara ya mafunzo katika Hifadhi za Taifa kwa lengo la kujijengea uwezo wa kitaaluma kuhusu rasilimali hizo.
Akizungumza na Storm Fm Mwakilishi wa walimu wa Sekondari kwenye Chama cha walimu Tanzania CWT wilaya ya Geita Mwalimu Gipson Petro amesema zaidi ya walimu 90 wamechangia kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.
Ametoa wito kwa walimu wa shule za msingi na sekondari pamoja na makundi mengine katika jamii ikiwemo madaktari kuchangamkia fursa hiyo kwani ziara hiyo inalenga kuwajengea uwezo wa kitaaluma kuhusu masuala ya uhifadhi.
Mwalimu Grassian Ntaleka wa Shule ya Msingi Igenge na Mwalimu Faraja Manyawa wa Shule ya Msingi Bombambili mjini Geita wamesema ziara hiyo itawasaidia kuwajengea uwezo wa kufundisha masuala yanayohusu maliasili na utalii.