Vijana wahimizwa kujikita katika kilimo cha kitalu nyumba
8 September 2023, 12:06 pm
Juhudi za kuendelea kuwahimiza vijana kujiingiza kwenye kilimo zinaendelea, kwani kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa, huku Kijani Consult wakija na njia mbadala kwa vijana wa Geita kutumia kilimo chenye mwanga mdogo wajua ili mazao kustawi vizuri.
Na Zubeda Handrish- Geita
Afisa kilimo kutoka halmashauri ya mji Geita Notikery Mwalongo, amewahimiza vijana kujikita katika kilimo, huku akikazia katika kilimo cha kitalu nyumba (Green House) na kuwakumbusha namna kilimo hicho kinachotumia kiasi kidogi cha mwanga wa jua kitakavyowaingizia kipato na kujikwamua kiuchumi .
Ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua vikundi vya wakulima wa nyanya kwa kilimo cha kitalu nyumba (Green House) vilivyoanzishwa na kusimamiwa na Kijani Consult Tanzania katika kata 5 ikiwamo ya Buhalahala, Ihanamilo na Nyanguku kwa halmashauri ya mji wa Geita huku Kamena na Bukoli ikiwa kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Geita.
Nae Mkurugenzi wa Kijani Consult Tanzania Mandolin Kahindi, amezungumzia dhamira yake ya kuanzisha mradi huo wa miezi 12 kwa gharama ya shilingi milioni 200, kwa kuwafundisha vijana vijana 200 njia mbalimbali za kufanya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabia nchi ili kujikwamua kiuchumi.
Nao wanufaika wa mradi huo wa Kijani Consult wamezungumzia manufaa ya mradi tangu kuanzishwa kwake katika vijiji vyao ikiwa ni miez 4 tu hadi sasa.
Kilimo cha Kitalu nyumba (Green House) mkoani Geita kilianzishwa na halmashauri ya mji wa Geita mwaka 2017 wakijenga vitalu nyumba 6, katika Kata ya Mgusu vikijengwa vitalu nyumba viwili, Kalangalala kimoja, Kata ya Nyankumbu kimoja, Bung’wangoko kimoja na Shiloleli kitalu nyumba kimoja huku wakiwasidia kuwaunganisha wananchi hao katika masoko, na Kijani Consult wakiendeleza juhudi za kuwakwamua vijana kiuchumi.