Mazingira FM

Kifo cha Loveness makambi ya Wasabato, mlezi asimulia

23 August 2025, 8:47 pm

Daniel Nyanza, Babu na mlezi wa mtoto Loveness Emmanuel Kilonzo aliyefariki kwenye makambi kijiji cha Mkula. Picha na Edward Lucas

Na. Edward Lucas.

Kijiji cha Mkula, Busega – Simiyu, kilikumbwa na simanzi kubwa tarehe 18 Agosti 2025, baada ya watoto watatu wa kike kufariki dunia ndani ya hema katika kambi ya watoto waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA).

Miongoni mwa waliopoteza maisha ni mtoto Loveness Emmanuel Kilonzo (9), ambaye kifo chake kimegusa mioyo ya wengi — si tu kwa sababu ya umri wake mdogo, bali pia kwa sababu ya safari yake ya mwisho kuelekea kambini.

Kwa mujibu wa maelezo ya babu yake, ndugu Daniel John Nyanza, Loveness hakuwa muumini wa SDA, bali wa Kanisa la AIC. Siku ya tukio, aliondoka nyumbani kimya kimya baada ya kutamani kuungana na rafiki zake waliokuwa wakielekea kwenye kambi hiyo.

Familia ilipojaribu kumzuia, alionekana mwenye msisitizo — akiona hakuna baya katika kushiriki jambo la kiroho na wenzake wa madhehebu tofauti.

Lakini ndoto hiyo fupi ya ushirika ilikatishwa ghafla.

Daniel John Nyanza, Babu na mlezi wa mtoto Loveness
Kushoto ni mtoto Pacience Yusuph na kulia ni Mary Desela

Loveness na wenzake wawili, Mary Dickson Desela (12) na Pacience Yusuph Lameck (14), walikutwa wamefariki ndani ya hema baada ya kutoka kwenye maombi ya alfajili saa 11:00 na kurudi kujifungia ndani ya hema kukiwa na jiko la mkaa

Kufuatilia tukio hilo mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha kwa kushirikiana na uongozi wa kanisa walisitisha makambi hayo na kutoa wito kwa viongozi wa dini na wananchi kutoa taarifa mapema kwa serikali kabla ya kuendesha makambi ili kuhakikisha usalama wa shughuli za makambi