

29 March 2025, 4:55 pm
Chama cha Mapinduzi Kata ya Salama kimefanya hafla ya kuwapongeza walimu wa Shule ya Sekondari ya Salama kwa mafanikio makubwa ya matokeo ya Kidato cha Nne 2024.
Na Adelinus Banenwa
Chama cha Mapinduzi Kata ya Salama kimefanya hafla ya kuwapongeza walimu wa Shule ya Sekondari ya Salama kwa mafanikio makubwa ya matokeo ya Kidato cha Nne 2024.
Chama hicho kimewapa walimu hati za pongezi kama motisha baada ya shule hiyo kufuta daraja sifuri katika matokeo ya mtihani.
Mkuu wa Shule, Rebecca Chambili, amesema mafanikio haya ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya serikali, walimu, na wazazi.
Amesisitiza kuwa shule hiyo imeonyesha mwendelezo mzuri wa matokeo kutoka 2022 hadi 2024, licha ya changamoto za upungufu wa walimu, vyoo, mashine ya kusaga chakula, mabweni, na uzio.
Afisa Taaluma wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Mariastellah Baltazari, alisema mikakati ya halmashauri, walimu, na wazazi imechangia mafanikio makubwa, huku akisisitiza umuhimu wa mazoezi na chakula cha wanafunzi shuleni.
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Pendo Masalu, alikishukuru Chama cha Mapinduzi kwa kutambua juhudi za walimu na shule.
Ameongeza kuwa juhudi za walimu zimechangia mafanikio haya ya ufaulu kwa 2024.
Shule ya Sekondari ya Salama ni mojawapo ya shule tano zilizofanikiwa kufuta daraja sifuri katika matokeo ya Kidato cha Nne 2024, kati ya shule 24 za serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Hafla hiyo ilihudhuriwa na zoezi la upandaji miti kwa ajili ya kutunza mazingira.