Mazingira FM

Mwalimu amsumbua mwanafunzi kimapenzi, mzazi amhamisha shule

21 July 2024, 8:27 pm

Mwanafunzi ahamishwa shule kuepuka kusumbuliwa na mwalimu aliyekuwa akimtongoza mara kwa mara

Na Thomas Masalu

Robert Chilare, mzazi wa mwanafunzi wa kike wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Mekomaliro, iliyoko kata ya Mihingo, wilaya ya Bunda, amemhamishia mtoto wake shule nyingine baada ya kuteswa mara kwa mara na mmoja wa walimu wa shule hiyo.

Mwalimu huyo alijaribu kumtongoza mwanafunzi huyo na alipoonywa, aliahidi kumpa adhabu kali mpaka atakapokubali ombi lake.

Chilare ameeleza malalamiko yake mbele ya Mbunge wa Jimbo la Bunda, Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, katika kikao cha kuangalia utekelezaji wa ilani ya Chama Cha mapinduzi CCM, katika kata ya Mihingo.

Wananchi katika mkutano ulioibua changamoto ya mzazi kumuhamisha mwanafunzi kisa kusumbuliwa na mwalimu akimtaka kimapenzi, Picha na Thomas Masalu

Chilare amesema alipopokea taarifa kutoka kwa mtoto wake kuhusu tukio hilo, alichukua hatua za haraka ikiwa ni pamoja na kufika shuleni na kuonana na Mkuu wa Shule.

Kikao cha dharura kilifanyika kilichohusisha Mkuu wa Shule, mzazi wa mtoto, Mratibu wa Elimu wa Kata, mwalimu anayetuhumiwa, walimu wengine wawili na mwanafunzi mwenyewe.

Mwanafunzi alieleza kuwa alikumbana na tukio hilo kama alivyoeleza mzazi, huku mwalimu akikiri wazi kuhusika katika suala hilo.

Sauti ya baba wa mwanafunzi

Kufuatia malalamiko hayo, Diwani wa kata ya Mihingo, Mheshimiwa Nyambura Nyamhanga, alisimama na kueleza kuwa amepokea taarifa za malalamiko ya mzazi huyo na hatua alizochukua.

Sauti ya Diwani

Mbunge wa Jimbo la Bunda, Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, amemshauri Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuchunguza suala hilo kwa umakini bila kumuonea haya mtu.
Getere amesema serikali ya awamu ya sita inataka watoto wasome na siyo kukatishwa masomo kwa sababu ya mtu mmoja.

Sauti ya Mbunge

Hata hivyo ofisi ya idara ya elimu secondari halmashauri ya wilaya ya Bunda kupitia kwa kaimu ofisa elimu secondari January Nzumba amesema watalifanyia kazi suala hilo haraka ili kuondoa taharuki iliyopo.

Sauti ya kaimu afisa elimu sekondari