Mazingira FM

Barrick North Mara watenga bil. 4.687 miradi mipya CSR

12 April 2025, 7:16 pm

Barrick North Mara umetenga kiasi cha shilingi bilioni 4.687 fedha ya uwajibikaji wa kampuni kwa wananchi CSR

Na Edward Lucas

Mgodi wa Barrick North Mara umetenga kiasi cha shilingi bilioni 4.687 fedha ya uwajibikaji wa kampuni kwa wananchi CSR kwa ajili ya miradi mipya ya maendeleo ndani ya halmashauri ya wilaya ya Tarime.

Hayo yameelezwa jana tarehe 11 Aprili 2025 na Meneja Mkuu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko mbele ya waandishi wa habari akizungumzia shughuli mbalimbali zinazofanywa na mgodi wa Barrick katika kuchangia maendeleo kwa wananchi.

Amesema ikiwa wanaendelea na utekelezaji wa miradi mingine yenye thamani ya shilingi bilioni 9.04 kwa uzalishaji wa mwaka 2023, tayari mgodi umetenga pesa zingine za CSR kutokana na uzalishaji wa mwaka 2024 kwa ajili ya miradi mipya ambapo kwasasa wako katika mchakato wa kuibua miradi hiyo na itakapokamilika wataitaarifu jamii kuwa ni miradi ipi.

Apolinary Lyambiko, Meneja Mkuu Barrick North Mara

Meneja Uhusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi amesema kama mpango wa utekelezaji wa CSR unavyosema asilimia 40 inakwenda katika vijiji 11 vinavyozunguka mgodi na asilimia 60 vijiji vingine ndani ya halmashauri wamepanga kuboresha huduma mbalimbali kama afya, elimu, miundombinu na mambo mengine ya uchumi wa wananchi.

Francis Uhadi, Meneja Mahusiano

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Genkuru, Juma Elias Kegoye amesema kutokana na mahusiano na mgodi kijiji kimeweza kuboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo elimu, afya na miundombinu ya barabara ambapo kwasasa tayari kijiji kimepokea kiasi cha zaidi ya bilioni 2 gawio la asilimia moja kwa maeneo ya uchimbaji waliyoyakabidhi kwa Barrick North Mara

Juma Elias Kegoye, mwenyekiti kijiji cha Genkuru