Waliopoteza maisha ajali ya Hiace Bunda yafikia 9
26 August 2024, 9:55 am
Idadi ya waliopoteza maisha katika ajali ya gari aina ya Hiace wilayani Bunda imefikia 9 huku majeruhi wakiendelea kupatiwa matibabu.
Na Adelinus Banenwa
Diwani wa kata ya Mugeta Mganga Jongora amesema tukio la ajali hiyo amezipata majira ya saa kumi kasoro jioni ya jana 25 Aug 2024 ambapo alipigiwa simu na mwenyekiti wa kijiji cha Kyandege.
Jongora amesema baada ya kupokea taarifa hiyo aliwasiliana na kituo cha afya Mugeta kwa ajili ya kupeleka gari la wagonjwa Ambulence ili kuwachukua majeruhi kuwawahisha kwenye huduma.
Jongora ameongeza kuwa pia aliwasiliana na jeshi la polisi pamoja an ofisi ya mkuu wa wilaya ya Bunda kuhusiana na tukio hiyo na alipofika kwenye eneo la ajali alikuta tayari watu saba tayari wamepoteza maisha.
Katibu tawala wilaya ya Bunda Salumu Mterela kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Bunda akizungumza na radio Mazingira Fm amesema ni kweli tukio hilo lipo ambalo limehusisha gari aina ya haice yenye namba za usajili T 942 CZG inayofanya safari zake kutoka Bunda kwenda Mugumu ambapo taarifa za awali zinaonesha chanzo ni mwendo kasi na taili la nyuma kupasuka.
Mterela amesema hadi sasa watu 9 wamethibitika kupoteza maisha na majeruhi wanaendelea na matibabu huku akisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi zaidi wa chanzo halisi cha ajali hiyo