Wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kutozwa fedha hospitalini ‘donda ndugu’
13 July 2024, 9:01 am
Suala la wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kupata huduma bure hospitali za umma bado ni donda ndugu kutokana na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi licha ya serikali kuendelea kusisitiza kuwa huduma kwa makundi hayo ni bure.
Na Adelinus Banenwa
Wananchi wa kata ya Kabasa halmashauri ya mji wa Bunda wamelalamikia suala la akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kutozwa fedha wanapokwenda kupata huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na wakati wa kujifungua kinyume na sera ya serikali.
Malalamiko hayo yametolewa kwenye mkutano wa hadhara wa Mhe mbunge wa jimbo la Bunda mjini Robert Chacha Maboto Kwenye kata ya Kabasa alipofika kuzungumza na wananchi na kusikiliza kero zao na namna gani wanaweza kuzitatua.
Wananchi hao wamemuomba mhe mbunge kuwasaidia kushughulikia Changamoto hiyo kwa kuwa imekuwa kawaida kwa watumishi wa afya kuwadai fedha wananchi wanaokwenda kupata huduma kwenye huduma ambazo serikali imezitaja kuwa ni bure.
Imedaiwa na wananchi hao kuwa akina mama wajawazito wanapokwenda kujifungua hudaiwa hadi shilingi laki 100,000 na hutakiwa kununua vifaa vya kujifungulia hata kama amekuja na vifaa vyake.
Akijibu hoja hiyo Mhe mbunge Maboto amesema jambo hilo hata bungeni limezungumzwa na halipendezi lakini pia bunge lilimuelekeza waziri wa afya kutuma walaka mwingine wa kukazia maelekezo yake ambayo pia kila mbunge apate nakala yake ili liweze kusimamiwa vizuri.