Mazingira FM
Mazingira FM
29 March 2026, 20:18

Utoaji elimu kwa wavuvi kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya uokozi utafuatiwa na ukaguzi wa kina katika maeneo ya uvuvi ili kuhakikisha sheria na taratibu za usalama zinazingatiwa.
Na Mwandishi wetu
Afisa Mfawidhi Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoa wa Mara, Hezroni Lusangija, amesema wavuvi watakaobainika kutovaa vifaa vya uokozi (life jacket) wanapokuwa majini watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kutozwa faini au kufikishwa mahakamani.
Akizungumza baada ya kutoa elimu kwa wavuvi kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya uokozi, Lusangija amesema pamoja na juhudi za mamlaka hiyo kutoa elimu, bado baadhi ya wavuvi hawazingatii maelekezo hayo muhimu kwa usalama wao.
Lusangija amesema baada ya zoezi hilo la utoaji elimu, mamlaka hiyo itaanza ukaguzi wa kina katika maeneo ya uvuvi ili kuhakikisha sheria na taratibu za usalama zinazingatiwa.
Wakizungumza mara baada ya kupatiwa elimu hiyo baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mtaa katika Kijiji cha Mkengwa, Kibuyi, Kinesi na maeneo ya jirani Wilaya ya Rorya, wameahidi kudhibiti vitendo vya baadhi ya wavuvi kufanya kazi kwa mazoea, hususan kutovaa majaketi ya uokozi wanapokuwa katika shughuli za uvuvi, jambo linalohatarisha usalama wa maisha yao.