Mazingira FM
Mazingira FM
8 March 2026, 13:21

Wanawake mkoani Mara wamehimizwa kutumia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kama fursa ya kujijengea uwezo wa kiuchumi kupitia shughuli za uhifadhi wa mazingira na uzalishaji wa mazao ya lishe
Na Catherine Msafiri,
Wanawake mkoani Mara wamehimizwa kutumia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kama fursa ya kujijengea uwezo wa kiuchumi kupitia shughuli za uhifadhi wa mazingira na uzalishaji wa mazao ya lishe, ili kuimarisha ustawi wa familia na jamii kwa ujumla.
Wito huo umetolewa wakati wa maadhimisho ya siku hiyo kimkoa yanayoendelea kufanyika katika Uwanja wa Sokoine wilayani Serengeti, ambapo mamia ya wananchi, wadau wa maendeleo pamoja na vikundi mbalimbali vya wanawake wamekusanyika kushiriki tukio hilo muhimu.

Katika hatua ya sasa ya maadhimisho hayo, mgeni rasmi ametembelea mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa na taasisi na vikundi mbalimbali vinavyojihusisha na shughuli za maendeleo ya wanawake na jamii kwa ujumla.
Miongoni mwa mabanda aliyoyatembelea ni banda la taasisi ya VI Agroforestry, linaloonesha shughuli mbalimbali wanazozifanya katika kuhifadhi mazingira na kuimarisha kilimo endelevu kwa jamii.
Akizungumza katika banda hilo, Bi. Mwajuma kutoka shirika la IDS Butiama amesema wanashirikiana kwa karibu na mashirika ya BUFADESO na MVIWANYA kwa udhamini wa VI Agroforestry, katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira pamoja na kuwajengea wanawake uwezo wa kuzalisha mazao ya lishe.
Maadhimisho ya International Women’s Day hufanyika tarehe 8 Machi kila mwaka, ambapo mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana ni Msingi wa Maendeleo Jumuishi kufikia Dira ya 2050.”