Mazingira FM

Kesi ya Kaunya na wenzake yaendelea leo mahakama ya Bunda

6 March 2026, 19:38

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Mheshimiwa Mulokozi Kamuntu.

Na Adelinus Banenwa

Kesi ya jinai namba 21 ya mwaka 2026 inayosikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda inaendelea kusikilizwa huku washtakiwa wakitetewa na mawakili wanne.

Upande wa utetezi unaongozwa na wakili msomi Dickson Matata anayewatetea washtakiwa namba 1 hadi 5. Wakili mwingine ni Alex Masaba anayewatetea washtakiwa namba 6 hadi 10. Aidha wakili Aloyce Kajitanus anawatetea washtakiwa namba 11 hadi 15 huku wakili Deogratius Mahinyira akiwatetea washtakiwa namba 16 hadi 21.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya makosa kumi likiwemo kosa la unyang’anyi kwa kutumia silaha, kufanya maandamano bila kibali, kumshambulia askari wa Jeshi la Polisi, pamoja na kuchoma moto majengo mbalimbali kinyume cha kifungu cha 319 (a) cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.

Aidha kosa la kumshambulia askari wa polisi linadaiwa kufanywa kinyume na kifungu cha 241 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, kinachohusu kumzuia au kumshambulia mtumishi wa umma akiwa anatekeleza majukumu yake.

Inadaiwa kuwa makosa hayo yote yalitendeka tarehe 29 Oktoba 2025.

Kesi hiyo imeendelea kusikilizwa leo ambapo mahakama iliendelea kupokea ushahidi kutoka upande wa mashtaka. Hadi kufikia sasa jumla ya mashahidi watano tayari wametoa ushahidi wao, huku mashahidi wawili wakisikilizwa leo ambao wote ni maafisa wa Jeshi la Polisi.

Sauti ya wakili Deogratius Mahinyira

Upande wa mashtaka umeieleza mahakama kuwa unatarajia kuwasilisha jumla ya mashahidi 41 katika kesi hiyo.

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Mheshimiwa Mulokozi Kamuntu, ambaye ameahirisha kesi hiyo hadi tarehe 9 Machi 2026 ambapo mahakama itaendelea kusikiliza ushahidi kutoka upande wa mashtaka.

Baadhi ya watuhumiwa katika kesi

Mara baada ya kesi hiyo kuahirishwa, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara John Wegesa Heche amesema kesi hiyo ni miongoni mwa kesi mbalimbali zilizofunguliwa dhidi ya baadhi ya wafuasi wa chama hicho nchini, ikiwemo kesi inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Tundu Antipas Mugwai Lissu.

Ametoa wito kwa serikali kuondoa kesi hizo mahakamani na kuruhusu chama hicho kuendelea na shughuli zake za kisiasa bila bughudha yoyote.

Amesema kazi ya CHADEMA na viongozi wake ni kuhakikisha wananchi wanapata haki, na hilo ndilo jambo ambalo chama hicho hakiwezi kuacha kulipigania.

Sauti ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara John Wegesa Heche