Mazingira FM
Mazingira FM
28 February 2026, 14:38

Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Mussa Hussein,akipokea vifaa mbalimbali ikiwemo madawati 248 na kompyuta 2 kwa ajili ya shule za msingi katika jimbo hilo.
Na Thomas Masalu
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Mussa Hussein, kwa niaba ya Mbunge wa jimbo hilo, Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, amepokea vifaa mbalimbali ikiwemo madawati 248 na kompyuta 2 kwa ajili ya shule za msingi katika jimbo hilo.
Katika mgawanyo huo, Shule ya Msingi Bukole imepatiwa madawati 129, Shule ya Msingi Mihare madawati 92, na Shule ya Msingi Nyamatoke madawati 27, yenye thamani ya jumla ya TZS 22,320,000.00.
Aidha, kompyuta hizo mbili zimegawiwa kwa Shule ya Msingi Mihare na Shule ya Msingi Nyamatoke, ambapo kila shule imepata kompyuta moja zenye thamani ya TZS 4,708,200.00.
Sambamba na hilo, umeunganishwa mtandao wa maji katika Shule ya Msingi Bukole wenye thamani ya TZS 2,906,400.00.

Vifaa hivyo vinalenga kunufaisha wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopakana na Pori la Akiba la Grumeti, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha sekta ya elimu katika Jimbo la Bunda Mjini.
Hafla ya makabidhiano imefanyika tarehe 27 Februari 2026 katika Shule ya Msingi Bunyunyi, Kata ya Hunyari, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mheshimiwa Aswege Enock Kaminyoge.
Akitoa salamu za Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, Katibu wa Mbunge, Mussa Hussein, ameshukuru Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) pamoja na Kampuni ya Grumeti Reserve kwa msaada huo.
Amesema hatua hiyo ni kielelezo cha ushirikiano mzuri kati ya wadau wa maendeleo na uongozi wa jimbo katika kuhakikisha watoto wa Bunda wanapata mazingira bora ya kujifunzia, pamoja na kuchochea maendeleo ya TEHAMA na ukuaji wa teknolojia kupitia kompyuta zilizotolewa.
Aidha, amewahakikishia wadau hao kuwa vifaa hivyo vitatunzwa vizuri ili viweze kuleta matokeo chanya na manufaa kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Katibu Hussein amesema kuwa Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, anaendelea kwa dhati kusimamia na kutafuta fursa mbalimbali za maendeleo kwa wananchi wake.
Aidha, amewasisitiza wananchi kuwa ofisi ya Mbunge ipo wazi wakati wote kwa ajili ya kuwasikiliza na kupokea maoni pamoja na changamoto zao, ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka na ufanisi.