Mazingira FM
Mazingira FM
30 August 2025, 12:40 pm

Mwandishi. Edward Lucas.
Masunga Mahala Mihayo (62), mkazi wa mtaa wa Ichamo, kata ya Kunzugu, Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara, amefariki dunia baada ya kushambuliwa na tembo katika maeneo ya kando ya Mto Rubana, ambako alikuwa akienda mara kwa mara kuokota kuni.
Peter Masamaki ambaye ni mjumbe na kaimu mwenyekiti wa mtaa wa Ichamo, amesema alipokea taarifa za tukio hilo tarehe 27 August 2025 majira ya saa 6 mchana baada ya wachungaji wa mifugo kuona mwili wa marehemu na kutoa taarifa ambapo walifika eneo la tukio na kuthibitisha kuwa mwili wa marehemu ukiwa hatua chache kutoka kando ya mto

Kwa upande wa wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Kunzugu, Lusasu Mwandu amethibitisha kuwa eneo hilo limekuwa likikumbwa mara kwa mara na matukio ya tembo kuvamia makazi ya watu.
Amefafanua kuwa licha ya jitihada zinazofanywa na baadhi ya taasisi za uhifadhi, bado hali si shwari na kuna haja ya kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha usalama wa wananchi wanaoishi jirani na mapori na hifadhi. Ameeleza kuwa serikali ya kata itatoa taarifa kwa ngazi ya juu ili hatua stahiki zichukuliwe.

Jeshi la Polisi pia lilifika eneo la tukio na kukamilisha taratibu zote za awali kabla ya kuukabidhi mwili wa marehemu kwa familia kwa ajili ya maandalizi ya mazishi. Polisi wamesisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona dalili za uwepo wa wanyama hatari katika maeneo yao.
Kwa mujibu wa mashuhuda, marehemu alionekana asubuhi ya siku hiyo akiwa salama alipokuwa akielekea kwenye eneo hilo la mto kuokota kuni, kama ilivyokuwa desturi yake.
Mmoja wa majirani na ndugu wa karibu wa marehemu,Amos Musa amesema alipokea kwa mshangao na huzuni kubwa taarifa za kifo hicho, hasa ikizingatiwa kuwa walizungumza na marehemu asubuhi ya siku hiyo. Ameeleza kuwa tukio hilo limeacha pengo kubwa kwa familia na jamii kwa ujumla.
