Mazingira FM
Mazingira FM
24 August 2025, 11:29 pm

“Kwa sasa hivi mimi ni mali ya chama sio tena mtu binafsi, kwahiyo taratibu zote….”
Mwandishi. Edward Lucas
Siku moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), tarehe 23 Agosti 2025, kutangaza rasmi majina ya wagombea ubunge kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, na kumtaja Ester Amos Bulaya kuwa mgombea wa ubunge wa Jimbo la Bunda Mjini, mwanasiasa huyo ameushukuru uongozi wa chama kwa kumuamini na kumpa fursa ya kupeperusha bendera ya CCM.
Akizungumza na Radio Mazingira FM, Bulaya amesema anatambua dhamana kubwa aliyopewa, na kwamba kwa sasa yeye ni mali ya chama hicho, hivyo atafuata itifaki na taratibu zote zilizowekwa na CCM.
Historia na Muktadha wa Kuteuliwa kwake
Uteuzi wa Bulaya umetokana na mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM, ambao ulikuwa na ushindani mkali katika Jimbo la Bunda Mjini. Katika hatua hiyo, Robert Maboto aliibuka kinara kwa kupata jumla ya kura 2,545, akifuatiwa na Kambarage Wasira aliyepata kura 2,032. Ester Bulaya alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 625. Hata hivyo, chama kupitia vikao vyake vya juu, kilimchagua Bulaya kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Bulaya si mgeni katika siasa za Bunda Mjini. Alianza kuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM kati ya mwaka 2010 hadi 2015, kabla ya kuhamia CHADEMA na kushinda Ubunge wa Bunda Mjini kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi wa 2015–2020.
Kuanzia mwaka 2020, aliteuliwa tena kuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chadema, lakini kipindi hicho kiligubikwa na mvutano mkubwa kati yake na chama hicho, pamoja na wenzake 18 waliokuwa kwenye mgogoro wa kikatiba na kisiasa na uongozi wa juu wa CHADEMA.