Nyumba yateketea kwa moto 20 wanusurika kifo Bunda
2 January 2025, 9:08 pm
Zaidi ya watu 20 katika mtaa wa miembeni kata ya Bunda stoo halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara wamenusurika kifo baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto.
Na Adelinus Banenwa
Zaidi ya watu 20 katika mtaa wa miembeni kata ya Bunda stoo halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara wamenusurika kifo baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto.
Kwa mujibu wa wahanga wa tukio hilo wanadai limetokea January 1, 2025 majira ya saa nne na nusu usiku ambapo wengine tayari walikuwa wamelala ndipo waliposikia kelele za moto na baada ya kushtuka walikuta moto umetanda nyumba nzima
Mwima Joktan miongoni mwa wapangaji ambaye inadaiwa moto huo ulianzia kwenye chumba chake ameiambia Mazingira Fm kuwa yeye alitoka kwenda kuoga nje lakini aliporudi alishangaa kukuta mlango wake ukiwa wazi na alipotaka kuingia ndani ndipo alipokuta moto umeshazingira chumba kizima
Mwenyekiti wa mtaa wa Miembeni Masalu Bukerebe amesema baada ya kusikia yowe majira ya usiku alikimbia hadi eneo la tukio kwa kushirikiana na wananchi wa mtaa huo walijaribu kila njia kuudhibiti moto huo ila ilishindikana
Bukerebe amesema hadi sasa haijajulikana chanzo cha moto huo ni nini huku akitoa rai kwa wananchi kuchukua tahadhari pindi wanapotumia moto na vifaa vya umeme pamoja na gesi kwenye nyumba zao.
Naye diwani wa kata ya Bunda stoo Mhe Flavian Chacha Nyamageko ametoa pole kwa wahanga wa tukio hilo pia amekabidhi kilo 100 za mchele kwa lengo la wahanga hao kupata chakula
Pia amemcshukuru mbunge wa jimbo la Bunda Mhe Boniphase Mwita Getere kwa kuwapa hifadhi wahanga hao ambapo baada ya kupewa taarifa juu ya tukio hilo Mhe Getere alitoa nyumba yake iliyoko jirani kwa wahanga kujihifadhi wakati wakifanya jitihada za kuyatafuta makazi mengine.
Flaviani ametoa rai pia kwa viongozi kuona umuhimu wa uwepo wa kikosi cha zimamoto na uokoaji ndani ya mji wa bunda kutokana na umuhimu wake hasa ukizingatia kupanuka kwa mji na matukio ya uokozi yanayotokea.