Mazingira FM

Esperanto sekondari yapokea vitabu vya kiesperanto

26 November 2024, 10:24 am

Walimu wanafunzi pamoja na wafadhili akiwa katika ukaguzi wa vitabu viliyoletwa shuleni hapo

Jumuiya ya waongeaji wa kiesperanto wamesaidia miradi kadhaa kwenye shule ya Sekondari Esperanto ikiwemo ujenzi wa mabweni mawili ya wanafunzi wa kike, maktaba ya vitabu na kompyuta, nyumba sita za walimu, matundu ya vyoo vya wanafunzi, madarasa na miradi mingine mingi.

Na Adelinus Banenwa

Zaidi ya vitabu 70 vya lugha ya kiesperanto vimekabidhiwa kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Esperanto iliyopo kata ya Ketare halmashauri ya wilaya ya Bunda Mkoani kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wa shule hiyo kujifunza zaidi lugha hiyo.

Vitabu hivyo vimetolewa na Dietrich Michael Wiedmann raia wa uswizi ikiwa ni sehemu ya kuwatia moyo wanafunzi hao ili waendelee kujifunza zaidi lugha hiyo.

Dietrich Michael Wiedmann raia wa Uswizi, akionesha sehemu ya vitabu alivyovileta

Rachel Busagi Masanga mwenza wa Dietrich Michael amesema kujifunza lugha ya kiesperanto kuna faida nyingi sana ikiwemo kupata marafiki kutoka kila pembe ya dunia hasa ukizingatia lugha ya kiesperanto haifungamani na taifa, rangi, kabila wa ukanda wowote duniani.

Rachel Busagi MASANGA akikabidhi moja ya vitabu kwa mwanafunzi shule ya sekondari Esperanto

Wanafunzi wa shule hiyo wameshukuru msaada huo wa vitabu uliotolewa na wageni hao ambapo wamesema vitawasaidia kuongeza uelewa kwenye kujifunza lugha hiyo.

Miongoni mwa vitabu vilivyokabidhiwa ni pamoja na vitabu vya historia ya lugha ya kiesperanto, kamusi ya lugha ya kiesperanto na kiingereza, vitabu vya kujifunza lugha ya kiesperanto ngazi ya awali miongoni mwa vitabu vingine.

wanafunzi shule ya sekondari esperanto wakifurahia pamoja na moja ya wafadhili aliyekabidhi vitabu vya lugha ya kiesperanto

Kwa upande wake Mramba Simba Nyamkinda ambaye ni makamu mwenyekiti wa waongeaji kiesperanto Tanzania amesema jumuiya hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha binadamu wote duniani wanakuwa sawa na ndugu.

Mramba Simba Nyamkinda makamu mwenyekiti wa waongeaji kiesperanto Tanzania akipokea vitabu kutoka kwa Rachel Busagi MASANGA

Aidha Mramba ameongeza kuwa jumuiya ya waongeaji wa kiesperanto wamesaidia miradi kadhaa kwenye shule ya Sekondari Esperanto ikiwemo ujenzi wa Mabweni mawili ya wanafunzi wa kike, Maktaba ya vitabu na Kompyuta, nyumba sita za walimu, matundu ya vyoo vya wanafunzi, madarasa na miradi mingine mingi.