Mazingira FM

Wanafunzi Chamtigiti kusomea chini ya mti, serikali yaweka mkono

11 August 2024, 9:47 am

George Stanley Mbilinyi, Mkurugenzi halmashauri ya wilaya ya Bunda.

Na Edward Lucas

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, George Stanley Mbilinyi, amesisitiza umuhimu wa kumalizia ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Chamtigiti, baada ya serikali kutenga shilingi milioni 50 kwa ajili ya madarasa mawili kupitia miradi ya EP4R na BOOST ili kusaidia kilio cha wanafunzi kusomea chini ya mti na wengine kupokezana darasa.

Amesema madarasa mawili yanayojengwa kwa msaada wa wananchi tayari yameshapelekewa andiko TAMISEMI na yanahitaji kumaliziwa kwa jumla ya milioni 25.

George Stanley Mbilinyi

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika tarehe 10 Agosti 2024, mbele ya Mbunge wa Jimbo la Bunda, Mheshimiwa Boniface Getere, Mwalimu Mkuu Emmanuel Godfrey Mahaga alieleza kuwa wanafunzi wa darasa la tatu wanalazimika kusoma chini ya mti kutokana na uchakavu wa darasa lao, na wanafunzi wa madarasa ya awali na la pili wanakumbana na upungufu wa madarasa.

Emmanuel Godfrey Mahaga, Mwalimu mkuu shule ya msingi Chamtigiti

Naye Mbunge wa jimbo la Bunda, Mhe. Boniface Mwita Getere amewasisitiza wananchi na viongozi wa eneo hilo kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa maboma ya madarasa mawili kwa hatua za nguvu za wananchi ili serikali imalizie hatua zitakazokuwa zimesalia

Boniface Mwita Getere, Mbunge jimbo la Bunda

Shule inahitaji madarasa 11, lakini ina madarasa 6 pekee, hali inayokwamisha shughuli za masomo.