Mazingira FM

Aliyekutwa anajisomea kwa mwanga wa taa za barabarani apewa zawadi

25 May 2024, 7:22 pm

Mhe Mkuu wa wilaya ya Bunda Dkt Vicent Naano na Furaha Hamis mwanafunzi wa shule ya sekondari Nyamakokoto.

Aliyekutwa akijisomea na kuandika notes kwa kutumia mwanga wa taa za barabarani huku akiuza karanga na miwa mjini Bunda usiku apewa zawadi na mkuu wa wilaya kama motisha.

Furaha Hamis mwanafunzi wa shule ya sekondari Nyamakokoto  aliyekutwa akijisomea chini ya taa za barabara usiku huku akifanya biashara alipiwa chakula shuleni mwaka mzima na kupewa vifaa vya shule na mkuu wa wilaya ya Bunda Dkt Vicent Naano.

Furaha ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Nyamakokoto siku chache zilizopita majira ya saa mbili usiku alikutwa akijisomea na kuandika notes chini ya taa za barabarani mjini Bunda huku pembeni akiendelea kufanya biashara ya kuuza karanga na miwa.

Mhe Mkuu wa wilaya ya Bunda Dkt Vicent Naano amesema wakati akiwa kwenye matembezi yake ya kawaida kwa miguu majira ya saa mbili usiku alimkuta mwanafunzi huyo jambo lililopelekea kufika shuleni anakosomea ili kumpatia zawadi kama motisha ya kusoma zaidi.

Furaha Hamis mwanafunzi wa shule ya sekondari Nyamakokoto akiwa anaandika notes huku akiendelea kufanya biashara.
Furaha Hamis mwanafunzi wa shule ya sekondari Nyamakokoto akiwa anajisomea huku akiendelea kufanya biashara.

Dc Naano amempatia zawadi ya madaftari, begi la shule pamoja na kalamu lengo ni kumtia moyo ili asome kwa bidii na kutimiza ndoto zake.

Mbali na zawadi hizo pia Mhe mkuu wa wilaya  amemlipia fedha ya chakula shuleni kwa mwaka mzima mwanafunzi huyo.

Mhe Mkuu wa wilaya ya Bunda Dkt Vicent Naano na Furaha Hamis mwanafunzi wa shule ya sekondari Nyamakokoto.

Kwa upande wake Furaha Hamis amemshukuru Mhe mkuu wa wilaya Dkt Vicent Naano kwa zawadi alizompatia ambapo amesema zitamsaidia kwenye kusoma huku akibainisha kuwa ndoto yake kubwa ni kuwa Rais wa Tanzania.