65% ya wanafunzi Bunda hufeli mtihani kidato cha nne
22 May 2024, 7:08 pm
Wazazi kutofatilia maendeleo ya watoto shuleni , utoro na ukosefu wa chakula shuleni chanzo cha wanafunzi wengi kufeli mtihani wilayani Bunda.
Na Adelinus Banenwa
Serikali wilayani Bunda chini ya mkuu wa wilaya dkt Vicent Naano imewasilisha utekelezaji wa ilani ya CCM Bunda huku kufeli kwa wanafunzi na ubovu wa barabara zikitajwa kama changamoto kubwa.
Dc Naano amesema serikali wilayani Bunda kwa July hadi Dec 2023 jumla ya miradi 196 imetekelezwa inayogharimu billion 210 ambapo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Suala lingine ni changamoto ya upande wa elimu ambapo DC Naano amesema asilimia zaidi ya 65% ya wanafunzi wilayani Bunda kwenye matokeo ya kidato cha nne hupata division 4 na sifuri
Aidha ametaja changamoto kubwa zinazopelekea matokeo hayo kuwa mabaya kuwa ni ukosefu wa chakula mashuleni, wanafunzi wengi kulelewa na bibi zoa badala ya wazazi, wazazi kutelekeza watoto shuleni bila ufuatiliaji pamoja na utoro wa wanafunzi miongoni mwa sababu nyingine.
Dc naano amesema ubovu wa barabara ni mkubwa katika mitaa na vijiji wilayani Bunda na hii ni kutokana na mvua kubwa za el-nino zilizonyesha tangu mwishoni mwa mwaka jana huku akiwatoa hofu wananchi baada ya mvua kuisha barabara zitaanza kutengenezwa kwa kuwa tayari fedha zipo na wakandarasi wameshachukua tenda.
Naye mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bunda ndugu Mayaya Abraham Magese amesema katika ziara ya kamati ya siasa ya wilaya kutembelea miradi jumla ya miradi 30 imekaguliwa na mradi mmoja umetembelewa.
Mwenyekiti Mayaya amesema mbali na miradi kuwa mizuri pia chama kimetoa maelekezo kwa serikali kikimtaka mkaguzi wa ndani kufanyia ukaguzi wa thamani ya fedha iliyotumika kujenga nyumba ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bunda na taarifa yake iwasilishwe kwenye chama.
Haya yamejili kwenye kikao maalumu cha halmashauri kuu ya CCM wilaya ya bunda kilichoketi kupokea utekelezaji wa ilani kwa mwezi July hadi Dec 2023.