BUWASSA watakiwa kutatua changamoto ya maji chuo cha ualimu Bunda
19 April 2024, 12:34 pm
Mwenyekiti wa CCM Bunda aitaka BUWASSA kutatua changamoto ya maji chuo cha ualimu Bunda.
Na Theresia Thomas
Wito umetolewa kwa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bunda BUWSSA kutatua changamoto ya upungufu wa maji safi chuo cha ualimu Bunda.
Wito huo umetolewa na mgeni rasmi Leonard Magwayega mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi chama cha mapinduzi CCM katika mahafali ya 38 ya chuo cha ulimu Bunda yaliyofanyika leo tarehe 18 April 2024 katika ukumbi wa chuo hicho.
Magwayega amesema changamoto ya upungufu wa maji katika chuo hicho haitakiwi kukaa muda mrefu pasipo kupatiwa ufumbuzi.
Katika hatua nyingine Magwayega amewataka wahitimu kuitendea haki elimu walioipata.
Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho Mwl Venance Mwita Mancheye amewataka wahitimu hao kujiajiri na kujitole sehemu zinazotoa huduma ya elimu ili kupata ujuzi, sifa na uzoefu wa taaluma waliyonayo.
Aidha ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha mazingira rafiki ya chuo na kuhudumia stahiki za watumishi wa chuo pamoja na wanachuo.
Awali akisoma risala ya wahitimu ngazi ya Stashahada na Astashahada mbele ya mgeni rasmi Kija Elias, amesema upungufu wa huduma ya maji katika chuo hicho imekua ikileta usumbufu kwa wanachuo hao.
Jumla ya wahitimu kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada ni 369, wasichana wakiwa 166 na wavulana wakiwa 203.