Ghala la pamba la 4C lateketea kwa moto Bunda
6 August 2023, 10:05 pm
Ghala la pamba linalomilikiwa na kampuni ya 4c limeteketea kwa moto huku likiwa na mzigo wa pamba ndani, hadi sasa haijulikani hasara ni kiasi gani.
Na Adelinus Banenwa
Katibu tawala wilaya ya Bunda Mhe Salumu Mtelela amesema hadi sasa haijulikani ni kiasi gani cha hasara kutokana na kuungua kwa ghala la pamba katika kiwanda cha 4c kilichoko eneo la viliani Bunda mjini.
Akizungumza katika eneo la tukio hilo Mhe Mtelela amesema yeye kama katibu tawala wilaya alipata taarifa kutoka kwa mkuu wa wilaya juu ya tukio la kiwanda cha pamba kuungua hivyo alichukua hatua za kuwasiliana na kikosi cha zimamoto na uokoaji ambao walifika na kuanza kazi ya kuzima moto huo.
Aidha amevishukuru vyombo vya usalama ikiwemo jeshi la polisi Bunda kwa kufika mapema kwa ajili ya kuweka ulinzi, pia kikosi cha zimamoto kwa kufika haraka kusaidia kutoa msaada wa kuzima moto huo ambao hadi sasa umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake kamanda wa zimamaoto na uokoaji mkoa wa Mara Agostino Magere amesema jeshi hilo limepata taarifa majira ya saa saba mchana na kikosi hicho kilifika mara moja kudhibiti moto huo.
Aidha Magere ameongeza kuwa changamoto ilikuwa ni maji hata hivyo viongozi wa Bunda walishughulikia changamoto hiyo kwa haraka ambapo amesema taarifa kamili itatolewa baada ya zoezi kukamilika.
Naye mkaguzi wa pamba wilaya ya Bunda Ndugu Hemed Kabea ameiambia mazingira Fm kuwa taarifa za kiwanda kuungua amezipata majira ya saa saba mchana lakini hatua mbalimbali zimefanyika kuhakikisha wanawasiliana na mmiliki wa kiwanda hicho ili kuona namna ya Kudhibiti moto huo .
pia ameishukuru ofisi ya mkuu wa wilaya ya Bunda pamoja na kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara kwa kuchukua hatua za haraka ili kupunguza madhara zaidi.