Ubovu wa barabara wasababisha ujenzi wa shule kusuasua Mihingo
10 January 2025, 10:59 am
Wasimamizi na mafundi kuwa mbali na eneo la mradi, ushiriki mdogo wa wananchi, ubovu wa barabara kati ya Mekomariro senta hadi kitongoji cha Nyansirori, chanzo cha kusuasua kwa ujenzi wa shule mpya ya msingi.
Na Mariam Mramba
Imeelezwa kuwa ushiriki mdogo wa wananchi, ubovu wa barabara kati ya Mekomariro senta hadi kitongoji cha Nyansirori, chanzo cha kusuasua kwa ujenzi wa shule mpya ya msingi katika eneo hilo.
Hayo yameelezwa na wananchi kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge wa jimbo la Bunda Mhe Boniphace Getere alipofika kusikiliza kero za wananchi katika kata ya Mihingo kijiji cha Mekomariro Jan 8, 2025
Aidha wananchi hao pia wamedai mradi huo umekuwa ukisuasua kutokana na wasimamizi na mafundi kuwa mbali na eneo la mradi.
Mwenyekiti wa kijiji cha mekomariro Juma Msanya amewataka wananchi wa kijiji hicho washirikiane kufanya kazi na wazabuni waliochukua kazi hiyo wapeleke viashiria kwa wakati pamoja na wasimamizi wa mradi huo wakae karibu na eneo la mradi.
Naye mbunge wa jimbo la Bunda Boniphace Getere ameitaka ofisi ya mkurugenzi kuteua msimamizi atakae kuwa eneo la kazi muda wote ili kusaidia mradi kwenda kwa haraka huku amewakemea baadhi ya wananchi wanaokwamisha shughuli za maendeleo.