Mazingira FM

Zimamoto Mara watoa tahadhari kuelekea sikukuu

18 December 2024, 7:09 pm

Mrakibu wa polisi Agustino Magere ambaye ni kaimu kamanda wa zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara

Jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara limewataka wananchi wote kuchukua tahadhari za usalama kuelekea sikukuu za kufunga mwaka 2024.

Na Adelinus Banenwa

Akizungumza kupitia kipindi cha Duru za habari ndani ya studio za radio Mazingira Fm Mrakibu wa polisi Agustino Magere ambaye ni kaimu kamanda wa zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara amesema ni wajibu wa wananchi wote kuchukua tadhari kipindi hiki kuelekea sikukuu za kufunga mwaka kutoka na kuwepo kwa shughuli nyingi ambazo bila tahadhari zinaweza kusababisha ajali

Ameainisha miongoni mwa tahadhari hizo ni pamoja na madereva kutopita kwenye madaraja yanayokuwa yamefunikwa na maji, kujaza mafuta kwenye vituo vya mafuta kukiwa na abilia ndani ya gari, kutumia simu kwenye vituo vya mafuta, kuacha watoto ndani peke yao bila mtu mzima kisha kwenda maeneo ya mikesha iwe ni kwenye nyumba za ibada au kwenye maeneo ya starehe, matumizi ya majiko ya mkaa usiku kwenye nyumba zisizotoa hewa miongoni mwa tahadhari zingine.

Aidha Kamanda Magere amewataka wananchi kutosita kutoa taarifa kwa jeshi la zimamoto na uokoaji pale matukio ya dharura yatakapojitokeza ikiwemo moto, kuzama kwenye maji na visima miongoni mwa dharura zingine.

Sauti Mrakibu wa polisi Agustino Magere ambaye ni kaimu kamanda wa zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara
SGT Samwel Kabati Fire Marshal mkoa wa Mara

Awali akizungumza na msikilizaji kupitia kipindi hicho cha Duru za habari SGT Samwel Kabati Fire Marshal mkoa wa Mara amesema moto unao vyanzo vingi lakini chanzo kikuu cha ajali za moto ni binadamu kupitia shughuli zake anazozifanya.

SGT Samwel amesema ndiyo maana kwa kiasi kikubwa jeshi la zimamoto na uokoaji linajikita zaidi katika utoaji elimu kwa wananchi kwa kuwa ajali za moto zilizonyingi zinatokana na shughuli zao.

Sauti ya SGT Samwel Kabati Fire Marshal mkoa wa Mara
Omary Mingange afisa habari na mahusiano wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara

Naye Omary Mingange afisa habari na mahusiano wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara amesema ni wajibu wa wananchi kutoa taarifa sahihi za matukio ya ajali au dharula zingine ili kuliwezesha jeshi la zimamoto na uokoaji kufika eneo la tukio na vifaa kulingana na mahitaji ya dharula husika

Samambamba na hilo amewashauri wananchi kutoa taarifa za moja kwa moja kuhusiana na matukio ya dharula yalipo iwe ni moto au kuzama ili kulisaidia jeshi hilo kufika bila kikwazo.

Aidha ameonya wale wote wanaotoa taarifa za uongo kupitia simu ya zimamoto ya dharula kuwa sheria iliyoliunda jeshi la zimamoto pia inavyo vifungu vya kumtia hatiani mtu yeyote atakayetoa taarifa za uongo kwa makusudi kwa jeshi hilo kwa kuwa matokeo ya uongo huo yanaweza kupelekea watu wengine kukosa huduma.

Sauti ya Omary Mingange afisa habari na mahusiano wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara