Mradi wa maji Wariku wa bilioni 1.6 watambulishwa rasmi
5 December 2024, 10:15 am
BUWSSA kutumia miezi sita kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa bilioni 1.6 kata ya Wariku mkurugenzi atoa tahadhari ya wizi wa vifaa.
Na Adelinus Banenwa
Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Bunda BUWSSA imetangaza kuanza kutekeleza mradi wa maji Wariku wenye thamani ya shilingi Bilion 1.6.
Akizungumza katika mkutano wa wananchi wakati wa utambulishaji wa mradi huo mkurugenzi mtendaji wa BUWSSA Bi Esther Gilyoma amesema tayari shughuli za utekelezaji wa miradi zimeanza ikiwa ni pamoja na ufikishwaji mabomba eneo la mradi, maandalizi ya ujenzi wa tenki lenje ujazo wa lita laki mbili (200,000) ambapo hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 8% ya utekelezaji wake.
Aidha mkurugenzi huyo amesema utekelezaji wa mradi huo uta chukua muda wa miezi sita hadi kukamilika kwake.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Bunda mjini Mhe Robert Chacha Maboto amesema wakazi wa kata ya Wariku wana kila sababu ya kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi hicho cha fedha ili kuwanufaisha wananchi wa kata hiyo ambapo ameongeza kuwa miradi hiyo inakuja kwa wananchi ni kutokana na juhudi mbalimbali za viongozi kuanzia kwa Diwani, Mbunge hadi kwa Rais.
Mhe Maboto amesema si mradi wa maji pekee ambao serikali ya awamu ya sita inatekeleza ndani ya jimbo la Bunda mjini pia ipo miradi mingine mbalimbali kama vile ujenzi wa shule ya Amali kata ya Sazira, ujenzi wa shule mpya ya sekondari kata ya Nyasura, pia zipo gari 2 za kubebea wagonjwa ( Ambulance) ambazo atazikabidhi muda wowote.
Kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Bunda Mhe Dkt Vicent Naano Anney katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela amewataka wananchi kutohujumu miundombinu ya serikali ambayo inaletwa kwenye maeneo yao kwa kuwa serikali inatumia gharama kubwa na yeyote atayejihusisha na hujuma hizo serikali haitomfumbia macho.
Kwa upande wao wakazi wa kata ya Wariku wameipongeza serikali na viongozi waliowezesha mradi huo kupatikana akiwemo diwani, mbunge pamoja na mkurugenzi wa BUWSSA ambapo wameeleza juu ya changamoto ya maji katika kata hiyo hasa kipindi cha kiangazi na kuhaidi kuilinda miundombinu hiyo.