Esperanto sekondari yapokea vitabu vya kiesperanto
26 November 2024, 10:24 am
Jumuiya ya waongeaji wa kiesperanto wamesaidia miradi kadhaa kwenye shule ya Sekondari Esperanto ikiwemo ujenzi wa mabweni mawili ya wanafunzi wa kike, maktaba ya vitabu na kompyuta, nyumba sita za walimu, matundu ya vyoo vya wanafunzi, madarasa na miradi mingine mingi.
Na Adelinus Banenwa
Zaidi ya vitabu 70 vya lugha ya kiesperanto vimekabidhiwa kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Esperanto iliyopo kata ya Ketare halmashauri ya wilaya ya Bunda Mkoani kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wa shule hiyo kujifunza zaidi lugha hiyo.
Vitabu hivyo vimetolewa na Dietrich Michael Wiedmann raia wa uswizi ikiwa ni sehemu ya kuwatia moyo wanafunzi hao ili waendelee kujifunza zaidi lugha hiyo.
Rachel Busagi Masanga mwenza wa Dietrich Michael amesema kujifunza lugha ya kiesperanto kuna faida nyingi sana ikiwemo kupata marafiki kutoka kila pembe ya dunia hasa ukizingatia lugha ya kiesperanto haifungamani na taifa, rangi, kabila wa ukanda wowote duniani.
Wanafunzi wa shule hiyo wameshukuru msaada huo wa vitabu uliotolewa na wageni hao ambapo wamesema vitawasaidia kuongeza uelewa kwenye kujifunza lugha hiyo.
Miongoni mwa vitabu vilivyokabidhiwa ni pamoja na vitabu vya historia ya lugha ya kiesperanto, kamusi ya lugha ya kiesperanto na kiingereza, vitabu vya kujifunza lugha ya kiesperanto ngazi ya awali miongoni mwa vitabu vingine.
Kwa upande wake Mramba Simba Nyamkinda ambaye ni makamu mwenyekiti wa waongeaji kiesperanto Tanzania amesema jumuiya hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha binadamu wote duniani wanakuwa sawa na ndugu.
Aidha Mramba ameongeza kuwa jumuiya ya waongeaji wa kiesperanto wamesaidia miradi kadhaa kwenye shule ya Sekondari Esperanto ikiwemo ujenzi wa Mabweni mawili ya wanafunzi wa kike, Maktaba ya vitabu na Kompyuta, nyumba sita za walimu, matundu ya vyoo vya wanafunzi, madarasa na miradi mingine mingi.