Mazingira FM

NMB yawapiga msasa matumizi ya fedha walimu zaidi 200 Rorya

13 September 2024, 9:46 am

Baadhi ya walimu walioshiriki katika Marsha

Walimu wanatakiwa kutumia fursa zinazowazunguka kubuni miradi mbalimbali ya kiuchumi hata kama wanamitaji midogo.

Na Adelinus Banenwa

Imeelezwa kuwa uoga wa kupata huduma kwenye taasisi rasmi za kifedha na ukosefu wa elimu juu ya matumizi sahihi ya mikopo nimiongoni mwa sababu zinazopelekea baadhi ya walimu kujiingiza kwenye mikopo umiza.

Hayo yamesemwa na baadhi ya walimu wilayani Rorya kwenye warsha iliyoandaliwa kwa ajili yao na benki ya NMB maarufu kama walimu spesho.

Walimu hao wamesema mikopo hiyo mbali na kuwarudisha nyuma kiuchumi lakini pia inawaathiri kisaikolojia na kijamii.

sauti za walimu
Meneja Mwandamizi Wateja Binafsi NMB, Ally Ngingite.

Akizungumza katika warsha hiyo, Meneja Mwandamizi Wateja Binafsi NMB, Ally Ngingite amesema benki hiyo imetambua changamoto zinazowakumba walimu ndio maana kundi hilo likapewa kipaumbele ambapo pamoja na mambo mengine walimu watapewa elimu ya ujasiriamali ili waweze kutumia fursa zinazowazunguka kwaajili ya kuboresha kipato chao.

Amesema umefika muda walimu wanatakiwa kutumia fursa zinazowazunguka kubuni miradi mbalimbali ya kiuchumi hata kama wanamitaji midogo na kwamba benki hiyo ipo tayari kuwawezesha kulingana na mahitaji yao huku akitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na uvuvi, kilimo na ufugaji.

Meneja Mwandamizi Wateja Binafsi NMB, Ally Ngingite
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya,  Abdul Mtaka.

Akifungua warsha hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya,  Abdul Mtaka ameishukuru benki hiyo kwa warsha  huku akisema warsha hiyo ni muhimu kwa kundi hilo ambalo ni kubwa miongoni mwa watumishi wa umma na kwamba hakuna mtumishi yeyote wa umma ambaye mshahara wake unatosheleza mahitaji yake.

Ameiomba benki hiyo kutoa elimu zaidi kwa walimu ili waweze kuelewa namna yakujikwamua kimaisha kupitia fursa zinazowazunguka badala ya kutegemea mishahara pekee.

Sauti ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya,  Abdul Mtaka

Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa,  Wogofya Mfalamagoha amesema warsha hiyo imewakutanisha walimu 200  kutoka wilaya ya Rorya ambapo pamoja na mambo mengine watapawa elimu ya fedha, ujasiriamali na kutoa maoni yao juu ya namna benki hiyo inavyotakiwa kuboresha huduma zake kwa kundi hilo.

Sauti Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa,  Wogofya Mfalamagoha