Wanafunzi 6 wapoteza maisha kwa kuzama bwawani Rorya
26 August 2024, 9:44 am
Wanafunzi sita wa shule ya msingi Ochuna wilaya ya Rorya mkoani Mara wamefariki dunia wakidaiwa kuzama na kunasa kwenye tope.
Na Adelinus Banenwa
Wanafunzi sita wa shule ya msingi Ochuna wilaya ya Rorya mkoani Mara wamefariki dunia wakidaiwa kuzama na kunasa kwenye tope katika bwawa la skimu ya kilimo cha umwagiliaji lililopo kijijini hapo.
Watoto hao wakiwemo watatu wa familia moja wote ni wakazi wa kijiji cha Ochuna.
Tukio hilo limetokea jana Jumamosi Agosti 24, 2024 jioni baada ya watoto hao kufika kwenye bwawa hilo kwa ajili ya kuogelea walipokuwa wanaendelea na kazi ya kuchunga mifugo.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka amesema wakiwa wanaogelea bwawani humo watoto hao walijikuta wakisogea hadi kwenye kina kirefu kisha kunasa kwenye tope.
Amefafanua kuwa miili yote imeopolewa na taratibu za mazishi zinafanyika kijijini hapo kwa uratibu wa serikali ya wilaya.
Kwa upande wake kamanda wa zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara Agostino Magere amesema taarifa za tukio hilo walizipata majira ya jioni ya jana hivyo kikosi cha zimamoto na uokoaji kutoka Tarime kilifika eneo la tukio na kuopoa miili hiyo ya watoto ambao tayari walikuwa wamepoteza maisha.
Akitaja majina ya watoto waliopoteza maisha katika tukio hilo kamanda Magere amesema
Aidha amewataka wananchi kuwa na tabia ya kutoa taarifa za majanga mapema kwa jeshi la zimamoto pindi majanga yanapotokea kuliko kuanza kufanya jitihada na pindi wanaposhindwa ndipo wanapokumbuka kutoa taarifa