DC Bunda azindua maktaba Esperanto sekondari
16 August 2024, 8:46 pm
Dkt Vicent Naano Mkuu wa wilaya ya Bunda amewataka wanafunzi kutumia vitabu hivyo kuongeza ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kufanya vizuri kwenye masomo yao.
Na Adelinus Banenwa
Mkuu wa wilaya ya Bunda Mhe Dkt Vicent Naano amezindua maktaba shule ya sekondari Esperanto ikiwa ni shule ya Sita kuwa na maktaba kwa halmashauri ya wilaya ya Bunda kati ya shule 24 zilizopo.
Maktaba hiyo yenye vitabu vya kiada na ziada imefadhiliwa na shirika la Stichting Mazingira, ambapo imetajwa kuwepo kwa maktaba hiyo kutasaidia wanafunzi kujisomea.
Katika uzinduzi huo Dkt Naano amewataka wanafunzi kutumia vitabu hivyo kuongeza ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kufanya vizuri kwenye masomo yao.
Mbali na uzinduzi wa maktaba pia Mhe mkuu wa wilaya amezindua darasa la Kompyuta lenye kompyuta tano zitakazotumika kwa mazoezi kabla ya kuanza rasmi somo hilo mwakani ambapo kompyuta hizo zimefadhiliwa na jamii ya waongeaji wa lugha ya Kiesperanto.
Mhe Mramba Simba Nyamkinda diwani wa kata ya Ketare amesema kupitia wafadhili na wadau mbalimbali shule hiyo imefanikiwa kupata miradi mbalimbali ikiwepo vyoo vya wanafunzi, bwalo la chakula, bweni la wanafunzi miongoni mwa miradi mingine.
Aidha Mhe Mramba amemuhakikishia mkuu wa wilaya kuwa usimamizi wa miundombinu na miradi inayofadhiliwa inakuwa salama na ifikapo mwakani shule hiyo itakuwa na kompyuta za kutosha kwa ajili ya kuanza rasmi somo la kompyuta.
Mariam Amos Mwanafunzi wa kidato cha nne amesema uwepo wa kompyuta shuleni hapo utasaidia kwa kiasi kikubwa kujifunza somo la TEHAMA ambalo tangu waanze kidato cha kwanza hawajawahi kujifunza somo hilo
Aidha Mariam amesema manufaa makubwa ya kujua kutumia kompyuta ni kuwa na fursa ya kujiajiri pindi unapomaliza shule.