Serengeti: Wamuua kikongwe kwa ahadi ya laki tano
20 January 2022, 10:31 am
Watu wanne akiwemo mwanamke mmoja wakazi wa kijiji cha Rigicha wanashikiliwa na Polisi wilaya ya Serengeti kwa tuhuma ya mauaji ya kikongwe kwa ahadi ya ujira wa sh500,000 wakimtuhumu kwa ushirikina.
Hata hivyo taarifa za awali zinadai kwamba hadi wanakamatwa walikuwa hajalipwa hizo fedha walizokubaliana kutekeleza mauaji hayo kwa kuwa zilitakiwa kutolewa baada ya kupukuchua mahindi na kuyauza.
Tukio hilo ambalo limeibua mjadala katika Kata ya Rigicha limetokea Januari 14 majira ya saa 2 usiku limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Longinus Tibishubwamu na kumtaja kikongwe huyo kuwa ni Wankuru Mwita (82) mkazi wa Kitongoji cha Mpakani.
Mwanamke huyo ambaye jina lake limehifadhiwa inadaiwa mwaka jana mme wake Sabasaba Nyamhanga alifungwa miaka 20 kwa kosa la ujangili na kumwacha mke na watoto hapo kwao chini ya mama mkwe wake.
Hata hivyo sababu za mwanamke huyo kutafuta genge la wauaji ni baada ya watoto wake watatu kuugua mara kwa mara kwa nyakati mbalimbali badala ya kuwapeleka hospitali akaenda kwa waganga wa kienyeji.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Rigicha Mkome Manyanya amesema,baada ya kufika eneo la tukio Mganga kutoka Zahanati ya Rigicha alifanya uchunguzi na kubaini kikongwe huyo alikatwa kwenye paji la uso na kwa nyuma na kitu cha ncha kali na damu nyingi zilivujia kitandani.