Mhe Maboto akabidhi meza 107 na shilingi laki tano na nusu sekondari ya Nyamakokoto
2 June 2024, 4:17 pm
Mhe Maboto “ili sehemu iwe na maendeleo inahitaji viongozi waadilifu katika kusimamia miradi na fedha zinazoletwa kwenye maeneo yao.”
Na Adelinus Banenwa
Mbunge wa jimbo la Bunda mjini mhe Robert Chacha Maboto amekabidhi meza 107 za wanafunzi shule ya sekondari Nyamakokoto na shilingi laki tano na nusu kwa ajili ya kuweka umeme shuleni hapo.
Akizungumza katika hafla hiyo Mhe Maboto amesema ili sehemu iwe na maendeleo inahitaji viongozi waadilifu katika kusimamia miradi na fedha zinazoletwa kwenye maeneo yao.
Ameongeza kuwa katika kipindi chake cha ubunge kwa kushirikiana na madiwa wa halamashauri ya Bunda mjini wamepata fedha nyingi za maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule ya kisasa ya sekondari Nyamakokoto na maeneo mengine, kukamilishwa kwa mradi wa chujio la maji Nyabehu, ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya mji pamaoja na vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali ndani ya jimbo la Bunda mjini.
Aidha Mhe Maboto ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanachagua watu sahihi katika chaguzi kwa kuwa uchaguzi wao ndiyo maendeleo yao.
Mbali na michango hiyo pia Mhe mbunge ameahidi kuchangia ununuzi wa mashine ya kurudufu mitihani (photocopy machine) pia ametoa mipira miwili kwa wanafunzi hao.
kwa upande wake diwani wa kata ya Nyamakokoto Emmanuel Machumu Malibwa amesema meza hizo 107 zilizokabidhiwa na mbunge zilipatikana kutoka kwenye fedha ya mfuko wa jimbo ambazo Nyamakokoto walipata shilingi million 5 hivyo pamoja na matumizi mengine waliamua kutengeneza meza hizo ili kupunguza uhaba wa meza shuleni hapo.
Kwa upande wake afisa elimu sekondari halamashauri ya mji wa Bunda Michael Mkoba, amemshukuru mbunge kwa kutoa fedha shilingi laki tano na nusu kuahakikisha huduma ya umeme inapatikana shuleni hapo pia amempongeza kwa kutoa fedha za kutengeneza meza za wanafunzi ambapo amesema zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza adha ya wanafunzi kuandikia kwenye magoti kutokana na ukosefu wa meza.
Mkoba amesema shule ya sekondari Nyamakokoto ina wanafunzi 601 ambapo kati yao wanafunzi 131 hawakuwa na meza kabisa hivyo kitendo cha kukabidhi meza hizo 107 kimesaidia kupunguza changamoto na sasa wanafunzi 24 ndiyo wamebaki bila meza za kuandikia.