BUWSSA: Mchakato wa kupeleka maji Nyasana umekamilika
24 May 2024, 12:38 pm
Wananchi watakiwa kushiriki kwenye miradi ya maendeleo inayokuja kwenye maeneo yao.
Na Mariam Mramba
Wananchi wa mtaa wa Nyasana kata ya Kabasa katika halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara wamesema wapo tayari kujitolea nguvu kazi zao kwa kushirikiana na BUWSSA katika kutekeleza mradi wa maji ambao unatarajiwa kutekelezwa Katika mtaa huo hivi karibuni.
Hayo yamesemwa katika mkutano wa hadhara uliolenga kuwaelimisha wananchi namna ambavyo wataweza kushiriki katika kutekeleza mradi wa maji ambapo wananchi hao wameiomba BUWSSA kuhakikisha mradi huo unakuwa wa uhakika nasio mradi wa kusuasua.
Kwa upande wake afisa mtendaji wa mtaa wa Nyasana Ferister Mbonamengi amesema kuwa wananchi wa mtaa huo wamekuwa na changamoto ya maji na wanawake wamekuwa wakiamka mapema sana kwenda kutafuta maji hivyo kwa mradi huo watashirikiana na BUWSSA kuhakikisha maji yanafika kila mtaa huo.
Akizungumza katika mkutano huo Mhandisi wa maji BUWSSA Mhandisi Vumilia Alex amesema kuwa mchakato wa kupeleka maji mtaa wa Nyasana umekamilika na zoezi la kutekeleza mradi huo utaanza kutekelezwa baada ya wiki mbili zijazo.
Diwani wa kata ya Kabasa Mhe Selemani Joseph amewaasa wananchi kushirikiana na BUWSSA kujitolea nguvu kazi zao na kuachana na dhana potofu kwamba kushiriki katika shughuli za maendeleo ni kuibiwa.