Hospitali ya mji wa Bunda yaanza kutoa huduma.
24 May 2024, 10:16 am
Kufunguliwa kwa huduma ya matibabu hospitali ya halmashauri ya mji wa Bunda inatajwa itapunguza adha kwa wakazi wa bunda stoo ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu.
Na Adelinus Banenwa
Diwani wa kata ya Bunda stoo Mhe Flavian Chacha Nyamageko ameendelea na ziara yake kwenye mitaa mbalimbali ndani ya kata yake ya Bunda stoo.
Mhe Flavian leo 23 May 2024 ametembelea hospital ya halmashauri ya mji wa Bunda ambayo imejengwa ndani ya kata yake ambapo hadi sasa serikali imetoa jumla ya shilingi bilion 2.3.
Katika ziara yake hiyo Mhe diwani akiwa ameambatana na mwenyekiti wa mtaa wa idara ya Maji Ndugu Mtaki Bwire ambapo amewataka wananchi wote wa kata ya Bunda stoo kwenda kupata huduma kwenye hospital hiyo maana huduma za wagonjwa wa nje (OPD) tayari zimeanza kutolewa hospitalini hapo.
Mtaki Bwire ambaye ni mwenyekiti wa mtaa wa Idara ya maji ameiambia Mazingira Fm kuwa uwepo wa hospitali kwenye mtaa wake utapunguza changamoto kubwa kwa wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Kwa upande wake Anna Asenga muhudumu wa afya hospital ya halmashauri ya mji wa Bunda amesema kwa upande wa akina mama huduma zinazotolewa ni pamoja na kuanzisha kliniki kwa akina mama wajawazito na watoto, kupima uzito, ushauri kwa akina mama, miongoni mwa huduma zingine.
Naye John Peter mganga mfawidhi hospitali ya halmashauri ya mji wa Bunda amesema hospitali hiyo imeanza kutoa huduma tangu tarehe 28 mwezi March mwaka huu 2024 na hadi sasa tayari wamehudumia wagonjwa zaidi ya 30.
Dr John amewataka wananchi wa Bunda stoo na maeneo jirani kwenda hospitalini hapo kupata huduma badala ya kwenda maeneo ya mbali maana tayari vifaa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa nje vinapatikana.