Mafuriko yawaweka hatarini wakazi wa Lamadi Simiyu
6 May 2024, 5:41 pm
Na Edward Lucas
Wananchi wa Kitongoji cha Makanisani na Lamadi kata ya Lamadi wilaya ya Busega mkoani Simiyu wako hatarini kupata milipuko ya magonjwa baada ya vyoo kujaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Wakizungumza na Mazingira Fm wakazi hao wamesema maji kutoka kwenye mito na mengine kutoka ziwani yasababisha baadhi ya vyoo na nyumba zilizokaribu na ziwa kuzama ndani ya maji na kupelekea wananchi kupaza sauti kwa kukosa makazi ya uhakika na salama
Kufuatia hali hiyo wananchi wametakiwa kutotumia maji ya ziwa na badala yake watumie maji ya bomba ili kuepuka magonjwa ya milipuko.
Mashimba Songoma ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Makanisani kata ya Lamadi amesema maji ya ziwani kwasasa sio salama na kuwasisitiza wananchi waliozoea kuchota maji kandokando ya ziwa na yale yaliyotuama katika maeneo yao waache kwani kuna huduma ya maji ya bomba iliyosambazwa katika miji yote ya kitongoji hicho ambayo ni salama zaidi kwa sasa.
Baadhi ya wananchi wamekiri kuwepo kwa maji ya uhakika kupitia huduma ya mabomba yaliyosambazwa katika maeneo hayo na kuliunga mkono agizo la viongozi kuzuia wananchi kutumia maji yalituama kwenye makzi yao kwani mengi yamechanganyika na majitaka kutokana na vyoo kuzama ndani ya maji