Ushirikiano na maslahi bora kwa walimu chachu kuongeza ufaulu Nyamakokoto
5 May 2024, 6:22 pm
Serikali ikizishughulikia changamoto za walimu na wazazi wakiwa na ushirikiano na walimu itasaidia kiwango cha ufaulu kitaongezeka.
Na Adelinus Banenwa
Wito umetolewa kwa wazazi na walezi kushrikiana na walimu pamoja na serikali ili kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi shuleni
Hayo yamebainishwa katika kikao cha kutathmini hali ya elimu kata ya Nyamakokoto kwa mwaka 2022 na 2023 kilichoitishwa na diwani wa kata ya Nyamakokoto Mhe Emmanuel Machumu Malibwa ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii halmashauri ya mji wa Bunda.
Kikao hicho kimewakutanisha walimu wa shule za msingi na sekondari za Nyamakokoto kamati ya siasa ya CCM kata ya Nyamakokoto, idara ya elimu halmashauri ya mji wa Bunda huku mgeni rasmi akiwa ni katibu tawala wilaya ya Bunda Salum Mterela kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Bunda.
Wakizungumza mbele ya mgeni rasmi walimu na wadau wa elimu wameeleza kuwa changamoto kubwa ni ushirikiano baina ya shule na wazazi jambo linalosababisha utoro kwa wanafunzi pia walimu kutopatiwa stahiki zao kwa wakati.
Michaeli mkoba afisa elimu ya watu wazima halmashauri ya mji wa Bunda kwa niaba ya mkurugenzi amesema ili kuinua taaluma kuna mambo lazima yazingatiwe ikiwa ni pamoja na ushirikiano baina ya wazazi na walimu, kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni, kukomesha utoro wa wanafunzi shuleni, walimu kutokamilisha silabasi miongoni mwa mambo mengine.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyamakokoto Emmanuel Machumu Malibwa amesema lengo la kuitisha kikao hicho ni kuzijadili changamoto zinazopelekea kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa shule za Nyamakokoto
Malibwa amesema walimu wakitimiza majukumu yao pia serikali ikizishughulikia changamoto za walimu na wazazi wakiwa na ushirikiano na walimu anaamini kiwango cha ufaulu kitaongezeka.