Tukosawa wahimiza utunzaji mazingira Bunda
19 April 2024, 4:47 pm
Madaraka Nyerere atembelea shule yenye jina la Nyerere awataka wanafunzi kutunza mazingira awahaidi kuwakaribisha Butiama.
Na Avelina Sulusi
Wito umetolewa kwa Jamii kutunza mazingira na kuyashika mafunzo katika utunzaji wa mazingira ili iwe faidi kwao kwa baadaye
Hayo yamesemwa na Madaraka Nyerere ambaye ni balozi wa mtandao wa Tukosawa alipotembelea shule ya msingi Nyerere ilayopo Bunda mjini ambapo amealikwa kama mgeni rasmi katika kikao cha Tukosawa ambao mtandao huo unajishughulisha na masuala ya utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nyerere Edwin Johakimu Byangwamu amesema mtandao wa tukosawa unaamini juu ya utu, upendo na umoja ambayo dhana yake kuu ni kwaajili ya kizazi cha sasa na kijacho katika kutunza mazingira.
Byangwamu amesema jumuiya ya tukosawa katika kutunza mazingira inaamini vitu vyote vilivyoumbwa katika dunia hii viko sawa na vinapaswa kutunzwa na kuendelezwa, amabapo amesema shughuli zilizofanywa na tuko sawa ni pamoja na kupanda miti ya matunda, vivuli, mbao , mbogamboga ambazo hutumiwa na wanafunzi na jamii nzima inayowazunguka.
Akisoma taarifa fupi juu ya changamoto wanazokutana nazo katika kutekeleza kazi za kikundi cha Green Rubana Women Group Bi Rose Costantine ambaye ni katibu wa kikundi hicho amesema anaomba kikundi chao kupata mafunzo na uzoefu kutoka vikundi vingine juu ya utunzaji wa mazingira.
Aidha ameiomba ofisi ya tukosawa kuweza kuendeleza ushirikiano ili shughuli za kikundi ziweze kuwapatia mbinu mbalimbali za ufanisi katika shughuli zao kwani shughuli zao zinategemea nguvu zao wenyewe.