Anayetuhumiwa kubaka, kulawiti mwanafunzi apandishwa kizimbani Bunda
21 March 2024, 7:20 pm
Bunda: Mwalimu aliyetuhumiwa kubaka, kulawiti mwanafunzi apandishwa kizimbani akana mashtaka arudishwa rumande
Na Adelinus Banenwa
Leo tarehe 21/03/2024 katika mahakama ya Wilaya Bunda amepandishwa kizimbani Vicent Joseph Nkunguu umri miaka 36 mwalimu mkuu shule ya msingi Masahunga kwa tuhuma za kujaribu kuua, kulawiti na ubakaji.
Kesi ya kwanza inayomkabili ni kesi namba 7623/2024 ambayo ni kujaribu kuua kinyume na kifungu cha 211 (a) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Kesi ya pili yenye makosa mawili ambayo ni kubaka kinyume na kifungu cha 130 (1), (2) (e) na kifungu cha 130 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022 na kulawiti kinyume na kifungu cha 154 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Awali akisoma mashtaka yanayomkabili mtuhumiwa huyo mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi wa mahakama Betron Sokanya , mwendesha mashtaka wa polisi Athuman Salimu alieleza mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 09/03/2024 majira ya usiku kwa kumbaka, kumlawiti na kujaribu kumuua kwa lengo la kupoteza ushahidi mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Masahunga (16) jina limehifadhiwa.
Katika kesi ya kwanza mshitakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwani mahakama haikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Na katika kesi ya pili mshtakiwa alikana makosa yote mawili ambapo hakimu aliamuru mtuhumiwa kurudishwa rumande hadi tarehe 03/04/2024 kesi hiyo itakapotajwa tena kwa kuwa mshtakiwa hakukidhi masharti ya dhamana.