Kambarage awapiga jeki sekondari ya Sizaki
20 October 2023, 10:36 pm
Kiasi Cha shilingi milioni 2 zimetolewa na Eng Kambarage Wasira Kwa ajili ya ukamilishaji wa choo shule ya Sekondari Sizaki.
Na Adelinus Banenwa
Kiasi cha shilingi milioni 2 zimetolewa na Injinia Kambarage Wasira kwa ajili ya ukamilishaji wa choo shule ya Sekondari Sizaki iliyopo kata ya Mcharo mjini Bunda. Kiasi hicho cha fedha kimetolewa katika mahafali ya 16 ya shule hiyo.
Katika hatua nyingine Injinia Kambarage amewataka wahitimu kuhakikisha wanafanya vizuri katika mtihani wao wa kuhitimu kidato Cha nne huku akitoa ahadi Kwa mkuu wa shule kusaidia kutafuta wadau kuhakikisha linapatikana jiko Kwa ajili ya kuandaa chakula Cha wanafunzi katika Mazingira salama.
Neema Michael Mkuu wa shule ya Sekondari Sizaki kupitia taarifa ya shule amesema shule hiyo imepata mafanikio mbalimbali tangu ianzishwe mwaka 2005 ikiwemo ujenzi wa bweni la wasichana na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Pamoja na mafanikio hayo pia amesema changamoto zinazoikabili shule hiyo Kwa Sasa ni ukosefu wa jiko la kuandalia chakula Cha wanafunzi, upungufu wa matundu ya vyoo Kwa wanafunzi miongoni mwa changamoto zingine.
Awali wakisoma risala mbele ya mgeni rasmi wahitimu wa kidato Cha nne shule ya Sekondari Sizaki wamesema walianza kidato Cha kwanza mwaka 2020 wakiwa jumla ya wanafunzi 181 ikiwa ni wavulana 72 na wasichana 109 lakini hadi leo wanahitimu wamebaki wanafunzi 120 miongoni mwao wavulana 49 na wasichana 71